Baadhi ya makazi ya wananchi wa Kijiji Cha Irkipusi kata ya Nainokanoka Wilaya ya Ngorongoro, Mkoani Arusha ambao wameiomba Serikali kuharakisha mchakato wa kuwahamisha katika eneo hilo la hifadhi.

Muktasari:

  • Wananchi wanaoishi ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro, katika Kijiji cha Irkipusi, Kata ya Nainokanoka, Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha wameiomba Serikali kuharakisha mchakato wa kuondoka katika hifadhi hiyo.

Ngorongoro. Wananchi wanaoishi ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro, katika Kijiji cha Irkipusi, Kata ya Nainokanoka, Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha wameiomba Serikali kuharakisha mchakato wa kuondoka katika hifadhi hiyo.

Wamesema wapo tayari kwenda popote kwa hiari yao na kwamba tangu mwaka jana serikali iliwaahidi kuwaondoa katika maeneo hayo kwa kuwapa fidia lakini bado hawajui hatima yao mpaka sasa.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi hao wamesema shughuli zao zimesimama kutokana na kusubiri kwa muda mrefu kuondoka katika maeneo hayo ilhali tayari wameshajiandikisha tangu mwaka jana.

Loiseriani Tormei, mmoja wa wananchi wa Kijiji hicho, amesema yupo tayari kwenda popote kama serikali itakamilisha mchakato huo kwa kuwa wamesubiri kwa muda mrefu tangu wajiandikishe mwaka jana.

"Tumejiandikisha tangu mwezi wa kumi mwaka 2022 mpaka leo hatujaondoka sijui ni kwanini, nyumba zetu zote zimeharibika maana hakuna uendelezwaji ambao tunafanya tukisubiri kuondoka na familia familia zetu," amesema.

"Binafsi nimekubali kuhama kwa hiari yangu mwenyewe kwenda popote na familia yangu wala sijalazishwa na mtu yoyote  kuondoka, ninachoomba kwa serikali itupe fidia zetu ili tuondoke Ngorongoro, sitaki nisubiri kuendelea kukaa hapa wakati nimeshajiandikisha, kuendelea kukaa hapa nikukwamisha mambo yangu maana siendi tena kazini kutafuta kibarua nimekaa nasubiri.

Norimoipoi Sapuro amesema  kwa kuwa wamekubali kuondoka kwa matakwa yao wenyewe ni wakati mwafaka sasa wa serikali kutekeleza makubaliano yao ili waondoke katika eneo hilo la hifadhi ili waweze kuendelea na shughuli zao kwa uhuru.

"Nimekubali kuhama na kwenda sehemu yoyote kwa matakwa yangu mwenyewe, lakini nataka serikali ituruhusu kwenda sehemu yoyote tunayotaka sisi wenyewe cha msingi serikali ituambie ni lini sasa tunaondoka Ngorongoro ili tupate fidia zetu tuondoke," amesema.


 David Laizer, ambaye ni mkazi wa Kata ya Nainokanoka ameishauri serikali katika kufanya wepesi wa jambo kuchukua vijana watano katika kila kata na kuwapa semina li watakaporudi waweze kuwaelimisha ndugu zao ambao hawajui lugha ya Kiswahili umuhimu wa jambo hilo.

"Tupo tayari kuhamia popote lakini mtupe semina hata kwenye kila kata watoke vijana watano tukaangalie maeneo tunayoenda je ni mazuri itasaidia watu kuelewa kwa haraka hili jambo, Sasa vijana hawa watakaporudi watawaelimisha wazazi wao na kwamba huko watakakokwenda ni pazuri na hakuna atakayekataa kuondoka," amesema.