Dar es Salaam. Kama ulitarajia kuiona Yanga popote kabla msimu haujaanza, umeumia. Kocha Miguel Gamondi amefuta uwezekano wa kuwepo kwa mechi yoyote ya kirafiki kubwa ambayo itahusisha mashabiki. Lakini ametoa sura ya soka ambalo vijana wake anataka walitambulishe pale mkoani Tanga dhidi ya Azam. Ile Yanga uliyoiona kwenye kilele cha wiki ya Mwananchi kama ulidhani ndio mziki wenyewe basi umekosea na sasa mabingwa hao wanacheza soka la tachi moja tu kisha unasogea, yaani pasi moja tu kisha tunakimbia haraka.

Falsafa ya Gamondi hataki mambo ya anaoanao sana labda uwe winga tu na unaingia ndani ya eneo la hatari lakini kwingine kote piga pasi moja kisha twende mbele.

Soka hilo limekuwa linawapa wakati mgumu mabeki wa timu pinzani katika mechi ambazo wameshacheza mpaka sasa wakiwa wanashindwa kuwakaribia wachezaji wa Yanga kuwazuia kutokana na pasi hizo za haraka ukiwa ndiyo mfumo wake.

Vita iko hapa:

Kama kuna maeneo ambayo Gamondi atakuwa na vita ya kufanya maamuzi ni eneo la kiungo na beki wa kati ambapo watu wote wako imara.

Pale beki wa kati Gamondi amelazimika bado kuendelea kuwasoma mabeki wake ambapo mabeki wote wanne nahodha wao Bakari Mwamnyeto, Dickson Job, Gift Fred na Ibrahim Hamad ‘Bacca’ wako sawa sawa ambapo tangu waanze kucheza mechi za kirafiki ukuta wao haujaruhusu bao hata moja.

Eneo lingine ni pale katikati ambapo Gamondi atakuwa na mtihani wa kuchagua viungo wa kucheza ambapo tangu Pacome Zouzoua alipoanza kucheza ameleta vita mpya.

Pacome amekuwa na moto mkali akicheza kama namba 10 akiongeza presha kwa Stephane Aziz KI huku pia Maxi Nzengeli licha ya kuwa anatumika kama winga wa kulia lakini pia amekuwa akionyesha makali akipewa nafasi ya kucheza eneo hilo kwenye mazoezi ambayo Mwanaspoti imeyashuhudia.

Kama kuna kitu ambacho Gamondi amewashtua mabosi wake ni uamuzi wake wa kugomea mechi za wazi kwa kikosi chake ambapo mabosi wa Yanga walitaka timu hiyo ikipige dhidi ya AS Vita ya DR Congo Jumapili, lakini akawaambia hakuna mchezo huo, labda upige Avic na hakuna shabiki kuingia.

Vita wako hapa nchini na jana walikuwa pale Singida wakicheza mchezo wa kirafiki dhidi ya wenyeji wao Singida Fountain Gate katika kilele cha siku yao lakini Gamondi akagomea wao kucheza Chamazi na Yanga.

Gamondi amewaambia mabosi wa Yanga kwamba atafutiwe mechi ngumu nyingine kwa timu ya ndani kisha wakipige kambini na sio Chamazi kwa kuwa atakuwa amekwenda kuuza silaha wakati Ngao ya Jamii ni wiki ijayo.

Tayari mabosi wa Yanga wameshachukua maelekezo hayo ambapo Mwanaspoti linafahamu huenda JKU wakashusha mjini kutoka Unguja Zanzibar kuja kujipima na mabingwa hao, na Jumapili hakutakuwa na mechi kama ilivyotangazwa awali. Yanga imepania kufanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa msimu huu.