Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara Yanga wameanza vizuri kampeni ya kutetea Ngao ya Jamii wakiichapa Azam FC kwa mabao 2-0.

Ushindi huo unaifanya Yanga Sasa kusubiri mshindi wa mchezo kati ya Simba dhidi ya Singida Fountain Gate kujua watakutana na timu ipi kwenye hatua ya fainali itakayopigwa Jumapili Agosti 13.

Yanga imetumia dakika 5 tu kuamua mchezo huo kwa mabao ya kiungo mshambuliaji Stephanie Aziz KI dakika ya 85 na mshambuliaji kinda Clement Mzinze dakika ya 89.

Mabadiliko ya kocha wa Yanga Miguel Gamondi dakika ya 65 akiwatoa Farid Mussa na Crispin Ngushi wakiingia Mzize na Azizi KI ndiyo yaliyotengeneza ushindi huo.

Aziz KI hilo ni bao lake la pili kuifunga Azam FC ambapo bao lake la kwanza aliwafunga katika mchezo wa Ligi msimu uliopita.

Gamondi ameanza msimu mpya wa rekodi nzuri akishinda mechi yake ya kwanza dhidi ya Azam huku mpinzani wake Yusuf Dabo akipoteza mchezo wa kwanza dhidi ya Yanga

Kipa wa Yanga Djigui Diarra amefanikiwa kutoka kwenye dakika 90 za pili dhidi ya Azam bila kuruhusu bao mechi zote zikichezwa Uwanja wa CCM Mkwakwani Tanga.