Muktasari:

  • Dada wa mwanamuziki maarufu duniani, Celine Dion, Claudette Dion ametoa maendeleo ya afya ya mwimbaji huyo anayepambana kutafuta matibabu ya ugonjwa wa Stiff Person Syndrome unaotajwa kutokuwa na dawa.

Dada wa mwanamuziki maarufu duniani, Celine Dion, Claudette Dion ametoa maendeleo ya afya ya mwimbaji huyo anayepambana kutafuta matibabu ya ugonjwa wa Stiff Person Syndrome unaotajwa kutokuwa na dawa.


Stiff Person Syndrome (SPS) ni hali adimu sana na isiyoeleweka, hupelekea ugumu wa misuli na kukakamaa, kuwa na mfadhaiko kwa muda kunatajwa kuchochea tatizo hilo.

Mwimbaji huyo wa kibao maarufu, My Heart Will Go On (1995), Desemba 2022 alitangaza kugundulika na ugonjwa huo ambao unaweza kusababisha ugumu wa misuli na mshtuko wa misuli.


"Hatuwezi kupata dawa ambayo inafanya kazi, lakini kuwa na matumaini ni muhimu." alisema dada wa mwimbaji huyo.

Hapo awali Insider waliripoti kuwa hakuna tiba ya ugonjwa huo lakini unaweza kudhibitiwa kwa kutumia sindano mahususi za kingamwili, dawa za kupunguza wasiwasi na vipumzisha misuli.

Msanii huyo mwenye umri wa miaka 55, Desemba mwaka uliopita katika video yake Instagram iliyogusa hisia za wengi alizungumzia ugonjwa huo.

"Nimekuwa nikikabiliana na matatizo ya afya yangu kwa muda mrefu. Imekuwa vigumu sana kwangu kukabiliana na changamoto hizi na kuzungumza juu ya kila kitu ambacho nimekuwa nikipitia." alisema.

"Hivi majuzi, nimegunduliwa kuwa na ugonjwa wa nadra sana wa neva unaoitwa stiff-person syndrome, ambao huathiri mtu mmoja kati ya milioni." alisema Celine Dion.

Ikumbukwe Celine anatambulika kuwa miongoni mwa wasanii waliouza sana duniani akiwa ameuza rekodi zaidi ya milioni 200, anachukuliwa kuwa mmoja wa waimbaji wa Pop waliofanikiwa zaidi.

Ameshinda tuzo tano za Grammy, ametunukiwa shahada mbili za heshima za udaktari wa muziki kutoka Chuo cha Muziki cha Berklee na Université Laval.

Mwaka 2008, Celine alitambuliwa kama msanii wa kimataifa aliyeuza zaidi nchini Afrika Kusini, kufikia mwisho mwa 2009, Celine alitambuliwa na Los Angeles Times kama msanii aliyeingiza fedha nyingi zaidi kwa muongo huo, kikiwa ni kitita cha Dola748 milioni.