📢Na ABIHA 📢

1. Alisema mahodari, mulohitimu shuleni,

Elimu ya sekondari, msingi kati na chini,

Ijayo tahadhari, kaka yenu nakupeni, 

 Chuo kikuu hatari, mukija muwe makini.


2. Wallahi si masihara, chuo kikuu hatari,

Kule Tanzania bara, na hata Zanzibari,

Dhambi zimetia fora, maovu yamekithiri, 

 Chuo kikuu hatari, mukija muwe makini.


3. Na hata nje ya nchi, popote pale uendapo,

Nako ni vurugu mechi, ingawa sijafikapo,

Walokwenda hawafichi, hutuambia warudipo, 

 Chuo kikuu hatari, mukija muwe makini.


4. Tunayaona matendo, wasomi na zao hulka,

Kutuletea mitindo, ya ajabu kwa hakika,

Ya watu kula vifundo, muwa ukatupwa taka, 

Chuo kikuu hatari, mukija muwe makini.


5. Nikueleze undani, niloyaona mwenzako,

Mazingira ya chuoni, hatari ilokuweko,

Hakika ni tafrani, ya watu mchanganyiko, 

Chuo kikuu hatari, mukija muwe makini.


6. Sikusudii kutisha, ili musije chuoni,

Bali nawafundisha mutambuwe, 

Sasa nayaainisha ndugu nisikilizeni, 

Chuo kikuu hatari, mukija muwe makini.


7. Huku kumeitwa chuo, kukapewa na ukuu,

Hakika mchanganuo, wa jina hili ni huu,

Zingatia kwa utuo, nitakayoyanukuu, 

Chuo kikuu hatari, mukija muwe makini.


8. Lolote ulitakalo, chuoni utalikuta,

Hata wacheza ndombolo, mauno wanayoyakata,

Na makundi kama hilo, ambayo yanafuata, 

Chuo kikuu hatari, mukija muwe makini.


9. Wanafunzi wa ajabu, ambao nawashangaa,

Wanaokesha vilabu, makasino na mabaa,

Chuo kikuu ni tabu, si pahali pa kukaa, 

Chuo kikuu hatari, mukija muwe makini.


10. Chuoni kuna uzinzi uliochupa mipaka,

Usaliti wa mapenzi, ya ndoa yakavunjika,

Chuoni kuna ushenzi, mwengine usiotajika, 

Chuo kikuu hatari, mukija muwe makini.


11. Marafiki mashetani, chuoni utawakuta,

Pamoja nao bwenini, chumba hwenda mukapata,

Watakubadili dini, endapo ukiwafuata, 

Chuo kikuu hatari, mukija muwe makini.


12. Niliyaona kwa macho, niliyonayo mawili,

Msichana wa Chokocho, aloshiba maadili,

Alipofika maficho, kule chuo Muhimbili, 

Chuo kikuu hatari, mukija muwe makini.


13. Alisimama Imara, mwanzoni alipofika, 

Vazi lake stara, nikabu kujifunika,

Ilimfika hasara, nalia nikikumbuka, 

Chuo kikuu hatari, mukija muwe makini.


14. Baada ya miezi saba, ni michache sio mingi,

Alipata maswahiba, wanafunzi mashangingi,

Wakamfanya kahaba, akayatupa mashungi, 

Chuo kikuu hatari, mukija muwe makini.


15. Binti alivyo sasa, siwezi kusimulia,

Ni nusu uchi kabisa, mavazi anayojitia,

Maisha yake ni visa, utupu anavyotembea, 

Chuo kikuu hatari, mukija muwe makini.


16. Na mwengine wa Muwambe, kaka wa Juma Nasoro,

Aliingia Mzumbe, chuo kipo Morogoro,

Ikawa wanywaji pombe, waovu masharobaro, 

Chuo kikuu hatari, mukija muwe makini.


17. Ndio marafiki zake, watenda vitendo hivi,

Na yeye hatima yake, kaambulia ulevi,

Kheri angekwenda chake, akawa muuza Duvi, 

Chuo kikuu hatari, mukija muwe makini.


18. Niwaongeze mmoja, kilembwe cha Bi Halima,

Wa Kaskazi Unguja, mzawa wa kule Kama,

UDSM alikuja,

Chuoni Daresalama, 

Chuo kikuu hatari, mukija muwe makini.


19. Kakutana na mzinzi, mbele ya Mola muasi,

Akadanganywa mapenzi, bila ya yeye kuhisi,

Mwishowe kaingia tanzi, akavikwaa virusi, 

Chuo kikuu hatari, mukija muwe makini.


20. Wengine toka mashamba, yaliyoko Tanganyika,

Mambo hayo ni sambamba, wengi nao yawafika,

Bali watoaji mimba, zijazo bila kutaka, 

Chuo kikuu hatari, mukija muwe makini.


21. Kuna vikundi vya dini, madhehebu teletele,

Wapiga kwaya bwenini, waimbao kwa kelele,

Tofauti za Iman, chuoni pia ni ndwele, 

Chuo kikuu hatari, mukija muwe makini.


22. Na fujo za matumizi, chuoni zinafanyika,

Simu saba na Ngamizi, na yasiyohitajika,

Hununua wanafunzi, vyumbani wakayaweka, 

Chuo kikuu hatari, mukija muwe makini.


23. Bwenini huwa ni zogo, watu kupiga miziki,

Si mkubwa si mdogo, kila mtu hashikiki,

Tafakari bwa mdogo, chuo kikuu ni dhiki, 

Chuo kikuu hatari, mukija muwe makini.


24. Kama unapenda ngoma, chuo kikuu ndio kwao,

Kila mwaka huririma kukaribisha wajao,

Mwaka wa mwanzo kusoma, ukarimu huwa kwao, 

Chuo kikuu hatari, mukija muwe makini.


25. Chuoni kuna uhuru, si kama kwenu kijana,

Ila wengi huwadhuru, kwa kuutumia sana,

Wakafika kukufuru, Imani wakazikana, 

Chuo kikuu hatari, mukija muwe makini.


26. Ukija kuwa makini, heshima na utiifu,

Jitambue wewe nani, upate uadilifu,

Hudhuria darasani, japo vipindi virefu, 

Chuo kikuu hatari, mukija muwe makini.


27. Jielewe jiamini, elimu jiongezee,

Kisha kumbuka nyumbani, walivyo wako wazee,

Wewe kwao tumaini, muda usiuchezee, 

Chuo kikuu hatari, mukija muwe makini.


28. Kamwe usiige watu, wachezao darasani,

Gemu na muvi si kitu, ushamba weka pembeni,

Elimu ndio wako utu, Akhera na Duniani, 

Chuo kikuu hatari, mukija muwe makini.


29. Namalizia kusema, kwa kushauri walezi,

Chuoni wendapo soma, wana na vyenu vizazi,

Waiteni kwa hekima, muwape habari hizi, 

Chuo kikuu hatari, mukenda muwe makini.

Chuo kikuu hatari, mukenda muwe makini.