Muktasari:

  • Kocha wa Manchester City amelaumu Bodi ya Kimataifa na Soka la Uingereza kwa kupitisha sharia ya kufidia dakika zilizopotea uwanjani bila kuwashirikisha wakati timu yake ikipoteza Ngao ya Jamii dhidi ya Arsenal.

London. Kocha Pep Guardiola ameishutumu kanuni mpya ya soka la England kutokana na bao la kusawazisha la Arsenal dakika ya mwisho lililoisaidia miamba hiyo ya London kutwaa Ngao ya Jamii.

Guardiola alisema mchezo haukutakiwa kumalizika haraka kiasi kile, akitania kuwa ungeweza hata kumalizika leo asubuhi kuanzia jana jioni, wakati kikosi chake kikipoteza kwa mikwaju ya penalti 4-1.

Bao hilo za kuzawazisha lilifungwa na mshambuliaji, Leandro Trossard dakika ya 11 ya nyongeza katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Wembley.

Dakika 16 na sekunde ya 34, zilizoongezwa katika mchezo huo ulikuwa mtindo mpya uliotumika kwa mara ya kwanza nchini England baada ya kuanza katika Kombe la Dunia, Qatar, ikiwa ni fidia kwa muda wote uliopotea wakati wa mchezo.

Lakini katika Uwanja wa Wembley, ziliongezwa dakika sita pekee, lakini muda uliongezeka baada ya ugomvi kati ya Kyle Walker na Thomas Partey, mwamuzi akiongeza nyingine saba.

Guardiola alisema: "Tunatakiwa kuzoea hili. Tulishinda bao 1-0. Nilidhani kwamba hakukuwa na matukio ya kuongeza dakika nane.

"Lakini ni sawali zuri kwa bodi za kimataifa za soka na kwa watu wote, kwa sababu hawashauriani kuhusu haya na makocha, hawashauriani na watu, wanakaa wenyewe,"

Ushindi huo wa Arsenal unakuwa muhimu zaidi kwa kocha Mikel Arteta, ambaye sasa ana mataji matatu tangu kutua Arsenal, ikiwamo Kombe la FA.

Lakini ni Man City pekee ambayo iliwahi kutwaa Ngao ya Jamii na kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu huo huo kwa miaka 12 sasa ya soka la England.