Dar es Salaam. Kiungo wa Clatous Chama amewataka mashabiki wao kukaa mkao wa kula kupata burudani kutoka kwao, kwani msimu huu watafanya vizuri.

Staa huyo ambaye alicheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Power Dynamos na Simba kushinda 2-0 alisema kila mchezaji anajua majukumu yake ya kuwepo katika timu hiyo na kufahamu inahitaji nini hivyo watapambana kuhakikisha wanatimiza.

Alisema kambi yao Uturuki ilikuwa nzuri na yenye faida kwa timu hivyo ni deni kwao kuhakikisha wanawapa kile wanachostahili mashabiki wao.

“Ushindani utakuwa mkubwa kwa kuwa kila timu inahitaji kupata matokeo na imesajili vizuri kukabiliana na ushindani. Nafikiri mashabiki wakae wakisubiri kuona tutawapa nini msimu huu kwa kuwa tumepania sana kuonyesha kiwango cha juu na naamini kuwa tutakuwa na timu bora,”alisema Chama na kuongeza kuwa msimu uliopita hawakuweza kupata mataji kama ilivyokuwa nyuma jambo linalowanyima usingizi wachezaji.

Huku Che Malone beki aliyesajiliwa kutoka Cotton Sports ya Cameroon akisema Simba ni timu kubwa hajaja kimakosa. Nimefurahi sana kuona wanasimba wengi na wanafurahia timu yao ni kazi kwetu wachezaji kuwapa matokeo mazuri hapa ni sehemu ya kuja kuwapa mafanikio mashabiki,”alisema staa huyo.