Summary

  • Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya SportPesa, Tarimba Abbas amesema wamekabidhi Sh405 milioni ikiwa ni sehemu ya makubaliano yaliyokuwepo katika mkataba walioingia na Yanga

KAMPUNI ya SportPesa ambao ni wadhamini wakuu wa Yanga, leo wameijaza noti klabu hiyo kwa kuipa bonasi ya Sh405 milioni kwa kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara, Ngao ya Jamii Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) na kutinga hatua ya fainali Kombe la Shirikisho Afrika.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya SportPesa, Tarimba Abbas amesema wamekabidhi Sh405 milioni ikiwa ni sehemu ya makubaliano yaliyokuwepo katika mkataba walioingia na Yanga

Tarimba amesema ni miaka sita sasa tangu wameingia mkataba na Yanga wanajisikia faraja kuingia mkataba na klabu ambayo inaipa heshima kubwa nchi kutokana na mafanikio makubwa wanayoyapata.

“Tanzania itakuwa sehemu ya wachezaji wengi kuja kucheza kutokana na mafanikio waliyoyafikia Yanga na timu nyingi kuendelea kunipa ila na wachezaji watakaokuja na sisi kama SportPesa tunasikia fahari.”

“Yanga kachukua Ngao, Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho Afrika ilibaki kidogo yanga kutwaa ubingwa Afrika kama sio fitna zilizofanyika.”

SportPesa tunaona fahari sana kwa jinsi Simba inatutoa kimasomaso, nembo ya Sportpesa kwa kupeleka mpira wa miguu kwenye ramani ya Afrika. Wanaitangaza SportPesa na ningewaomba wazidi kufanya vizuri zaidi kwani ni faraja kwetu.”

Tarimba alisema ameridhishwa na mikakati wanayoifanya anatarajia mambo makubwa msimu ujao na wao kama wadhamini wanaona mataji mengine msimu ujao.

Rais wa Yanga, Hersi Said amesema anawashukuru SportPesa na kuwaahidi kuwa wataendelea kuwa wawakilishi wao kwa kufanya yaliyo bora zaidi.

“Mafanikio tuliyoyapata yanachangiwa kwa kiasi kikubwa na SportPesa kutokana na mkataba wao kuendelea kutekeleza makubaliano yetu yaliyokuwa kwenye mkataba.” amesema Hersi ambaye ametimiza mwaka mmoja tangu ameingia madarakani.