Summary

  • Morrison anayesifika kwa kuchekesha lakini akiwa na uwezo mkubwa wa kusakata kabumbu, alitokeza ghafla ndani ya kikosi cha Rajaa FC kiichokuwa na mchezo dhidi ya Kibangu Rangers iliyokuwa na nyota mwingine wa zamani wa Yanga, Said Juma Makapu.

Baada ya kuachwa na Yanga, winga wa zamani wa Simba, Benard Morrison amegoma kuondoka Tanzania na ameonekana akicheza mechi ya Ndondo kwenye Uwanja wa Air Wing, Dar es Salaam.

Morrison anayesifika kwa kuchekesha lakini akiwa na uwezo mkubwa wa kusakata kabumbu, alitokeza ghafla ndani ya kikosi cha Rajaa FC kiichokuwa na mchezo dhidi ya Kibangu Rangers iliyokuwa na nyota mwingine wa zamani wa Yanga, Said Juma Makapu.

Kama kawaida yake, winga huyo machachari aliyekuwa amevalia jezi namba 16 alitoa burudani katika mechi hiyo na kuwa kivutio kwa mashabiki wengi waliojitokeza uwanjani hapo kutokana na aina yake ya kucheza na vichekesho vyake vya hapa na pale.

Hakuishia hapo, Morrison aliisaidia timu hiyo ya mtaani kuibuka na ushindi wa mabao 2-1, mbele ya Kibangu ya akina Makapu, huku ikielezwa alivuta mkwanja usiopungua Sh300,000 ili kuvaa jezi ya Rajaa.

Hiyo, ilikuwa kama mazoezi kwake, lakini Mwananchi linajua yupo Dar es Saalam akikamilisha uhamisho wake wa kujiunga na Singida Fountain Gate na kama kila kitu kitakwenda sawa msimu ujao atawatumikia Walima Alizeti hao wa Kanda ya Kati.

Msimu uliomalizika, Morrison alikuwa na kikosi cha Yanga akiisaidia miamba hiyo kwenda fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, huku ikitwaa taji la Ligi Kuu Tanzania Bara, Ngao ya Jamii na Kombe la FA (ASFC).