Summary

  • Timu zote zilizomaliza nafasi nne za juu zimeanza mambo. Simba  na Yanga ziko kwenye hatua ya mwisho la kukamilisha usajili wao na muda wowote kuanzia leo vifaa vitaanza kupishana kwenye Viwanja vya ndege kuwasili Dar.

NI suala la muda tu Ligi Kuu Bara itaanza rasmi mwezi ujao kwa timu 16 kutafuta bingwa wa msimu wa 2023/2024. Tayari baadhi ya timu zimeshaanza kukiwasha baada ya mapumziko ya zaidi ya mwezi mmoja kupita.

Mwezi huu ni muhimu zaidi kwa timu zote, kwani ndiyo mwezi ambao kila timu itaanza harakati zake, lakini ndiyo ule ambao utaonyesha picha ya msimu ujao.

Timu zote zilizomaliza nafasi nne za juu zimeanza mambo. Simba  na Yanga ziko kwenye hatua ya mwisho la kukamilisha usajili wao na muda wowote kuanzia leo vifaa vitaanza kupishana kwenye Viwanja vya ndege kuwasili Dar.

Simba jana ilifanya vipimo vya afya kwa mastaa wao  12 wazawa waliosaliwa nao kikosini. Lakini leo mastaa tisa wa kigeni wakiongozwa na Jean Baleke watafanyiwa vipimo pamoja na kipa mzawa, Aishi Manula. Mapro hao ni Baleke, Henock Inonga, Joash Onyango, Sadio Kanoute, Chama, Moses Phiri, Saido, Peter Banda na Sakho.

Huko Yanga nako wiki hii watafanya hivyohivyo, huku Kocha Miguel Gamondi akitegemewa kuja na sapraizi kubwa kikosi hapo kwa maana ya benchi lake ni jipya pamoja na angalizo alilotoa kwa viongozi.

Habari za ndani zinasema kwamba hata viongozi wa Yanga wanategemea sapraizi kubwa kwa Gamondi kwani kinyume na matarajio yao kila anachofanya amekuwa akizingatia sana umri wa mchezaji husika na ameshakagua mafaili ya mastaa wote na kutoa msimamo.

Mmoja wa viongozi wa usajili wa Yanga alisema kwamba hata katika mastaa wapya waliosajiliwa amewabana sana kwenye umri kutokana na aina ya soka lake na mipango yake kwenye Ligi ya Mabingwa, jambo ambalo huenda likaona wachezaji wengi wenye umri mdogo wakipewa nafasi. 

Singida na Azam na wenyewe wameshaanza vipimo kwenye maeneo mbalimbali huku kila mmoja akipania kufanya vizuri kwenye Ligi pamoja na Kombe la Shirikisho linaloanza Agosti 18. Mambo haya yatachangamsha nchi mwezi huu;

USAJILI:

Julai Mosi, usajili wa Ligi Kuu Bara ulifunguliwa na timu zote kupewa rungu la kushusha majembe yao ili kuhakikisha kuwa zinakuwa na kikosi imara msimu ujao.

Tayari Azam FC wamekuwa wa kwanza kutangaza majina ya wachezaji wao wawili wapya kiungo mshambuliaji Gibril Sillah, kiungo Feisal Salum  na inaelezwa kuwa watashusha wengine wawili muda wowote kabla ya kambi ya Tunisia.

Vurugu za Simba na Yanga ndizo zinazotazamiwa kwa wingi kuanzia leo Jumanne ambako habari za ndani zinasema timu hizo zimeshakamilisha kwa siri sana usajili wao mpya imebaki kuwashusha tu Dar es Salaam.

Yanga wamehusishwa na mastaa wengi wakubwa, lakini baadhi ni Jonas Mkude ambaye ameachwa na Simba, Nickson Kibabage ambaye anatokea Singida Fountain Gates na wengine wengi. Uwanja wa ndege utakuwa bize.

Miongoni mwa watu wanaosubiriwa kwa hamu Simba ni kipya mpya Caiquez Santos, mabeki Willy Onana na Chedoh Malone ndiyo ambao wanatajwa sana.

KUPIMA AFYA NA MAKOCHA

Tumeshaona timu za Azam na Simba zikiwapima wachezaji wao afya jana, Simba walikuwa Hospitali ya Muhimbili, huku Azam wakiwa Agakhan Hospital, bado tunasubiri kuziona timu nyingine ikiwemo Yanga zikiwachukua wachezaji wao na kuwapeleka kufanya zoezi hilo, zoezi ambalo hufanyika kabla msimu haujaanza.

Kocha wa Simba, Olivier Robertinho yupo Brazil ameshasema kuwa atatua hapa nchini kabla ya Julai 10, kwa ajili ya kuanza maandalizi ya msimu mpya wa ligi na yule mpya wa Yanga, Miguel Angel Gamondi yupo kwa Argentina, anashuka hapa nchini kabla ya Julai 15.

KAMBI MPYA

Tayari imeshafahamika kuwa timu zote mwezi huu zitaanza maandalizi kwa ajili ya msimu ujao, msimu uliopita timu za Simba na Azam na nyingine ikiwemo Geita zilitoka nje ya nchi kwa ajili ya maandalizi, lakini Yanga hawakutoka na walitwaa makombe yote.

Inadaiwa kuwa baadaye mwezi huu Simba wataondoka na kuweka kambini nchini Uturuki kwa ajili ya kutafuta makali ya msimu ujao, huku Azam wakitajwa kuwa wataondoka na majembe yao kwenda kuweka kambi nchini Tunisia.

Yanga bado hawajasema wanakwenda wapi lakini mwezi huu ndiyo watawatangazia mashabiki wao kama wanatoka au wanatufutia dawa ya msimu ujao, Avic pale Kigamboni kama msimu uliopita.


JEZI MPYA

Tayari maswali kuhusu jezi za Simba, Yanga kwa ajili ya msimu ujao yamekuwa mengi sana, tayari Simba wameshasema kuwa mwanzoni mwa mwezi huu jezi zitaanza kutoka, sawa na kauli ambayo imetolewa na Yanga.

Tofauti na ilivyokuwa msimu uliopita ambao jezi za Simba zilichelewa na zile za Yanga zikawahi, msimu huu inaonekana kuwa ndani ya mwezi huu kila timu jezi zake zitakuwa zimeshatoka na mashabiki kuanza kutamba nazo mtaani.

Ikiwa inaelezwa kuwa Ligi Kuu Bara itaanza mwezi ujao, hadi sasa bado ratiba ya ligi haijatolewa ili kila timu kufahamu kuwa itaanza na nani.

Pamoja na ratiba hiyo kuwa bado, mashabiki wa Singida, Simba, Yanga na Azam bado hawajafahamu mfumo mpya wa mashindano ya Ngao ya Jamii utachezwaje na nani ataanza na nani.

Hayo nayo ni mambo ambayo yatatangazwa na bodi ya Ligi Kuu Bara ndani ya mwezi huu ili timu ziwe na angalau wiki kadhaa za kujiandaa kabla ya ligi. Julai ndio hii, acha kiwake.


Â