JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

OFISI YA RAIS - TAMISEMI

TAARIFA KWA UMMA

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU ZOEZI LA UCHAGUZI WA WANAFUNZI WA

KUJIUNGA NA KIDATO CHA TANO, VYUO VYA UALIMU, VYUO VYA ELIMU YA

UFUNDI NA KATI KWA MWAKA 2023


Ndugu Wanahabari;

Zoezi la Uchaguzi wa Wanafunzi wa Kujiunga na Kidato cha Tano katika

Shule za Sekondari, Vyuo vya Ualimu, Vyuo vya Elimu ya Ufundi na Kati vya

Serikali Mwaka 2023, limekamilika. Zoezi hili limefanyika kwa kuzingatia

takwimu za matokeo ya Wanafunzi waliofanya Mtihani wa Kidato cha Nne

Mwaka, 2022, kutoka Tanzania Bara. Wanafunzi waliochaguliwa ni kutoka

Shule za Serikali, zisizo za Serikali, watahiniwa wa kujitegemea waliofanya

mtihani chini ya Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima na Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi.


Ndugu Wanahabari;

Matokeo ya Mtihani wa Kidato cha Nne mwaka, 2022 yanaonesha kuwa

Watahiniwa 192,348 (36.95%) walipata ufaulu wa Daraja la I – III. Kati ya hao

Tanzania Bara walikuwa watahiniwa 188,128 wakiwemo wasichana 84,509

na wavulana 103,619. Wanafunzi hawa wote wamekidhi vigezo vya kujiunga

na Kidato cha Tano, Vyuo vya ualimu,Vyuo vya Elimu ya Ufundi na Kati kwa

mwaka, 2023. Idadi hii inajumuisha Wanafunzi wenye Mahitaji Maalum 490

ambao wasichana ni 218 na wavulana ni 272.

Wanafunzi wote 188,128 waliokidhi vigezo wamechaguliwa na kupangiwa

kujiunga na Kidato cha Tano katika shule mbalimbali nchini pamoja na Vyuo

vya fani mbalimbali kama ifuatavyo:

(a) Wanafunzi 129,830 wakiwemo wasichana 66,343 na wavulana 63,487

sawa na asilimia 69 ya wenye sifa, wamechaguliwa kujiunga na Shule za

Sekondari za Kidato cha Tano 540 zikiwemo Shule mpya 29 zinazoanza

mwaka huu wa 2023 kwa mchanganuo ufuatao.

(i) Wanafunzi 1,878 wakiwemo wasichana 1,097 na wavulana

781 wamepangiwa katika Shule za sekondari Maalum 8 za

Kilakala, Mzumbe, Ilboru, Kisimiri, Msalato, Kibaha, Tabora Boys na Tabora Girls.

(ii) Wanafunzi 122,908 wakiwemo wasichana 62,731 na wavulana

60,177 wamepangiwa katika shule 519 za Sekondari za Bweni za Kitaifa za Kidato cha Tano.

(iii) Wanafunzi 5,044 wakiwemo wasichana 2,515 na wavulana 2,529

wamepangwa katika Shule 11 za Sekondari za Kutwa za Kidato cha Tano.

(b) Wanafunzi 58,298 wakiwemo wasichana 18,166 na wavulana 40,132

sawa na asilimia 31 wamepangiwa kujiunga kwenye kozi mbalimbali

za Stashahada katika Vyuo vya Kati vinavyosimamiwa na Baraza la

Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTVET) katika mchanganuo ufuatao:

(i) Wanafunzi 1,645 wakiwemo wasichana 646 na wavulana 999

wamechaguliwa kujiunga na Vyuo vya Ualimu ngazi ya Stashahada ya Sayansi, Hesabu na TEHAMA.

(ii) Wanafunzi 1,877 wakiwemo wasichana 757 na wavulana 1,120

wamechaguliwa kujiunga na fani mbalimbali katika Vyuo 04 vya Elimu

ya Ufundi ambavyo ni Chuo cha Ufundi cha Arusha (ATC), Taasisi ya

Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Chuo Kikuu cha Sayansi na

Teknolojia Mbeya - MUST na Chuo cha Usimamizi na Maendeleo ya Maji (WDMI).

(iii) Wanafunzi 1,842 wakiwemo wasichana 943 na wavulana 899

wamechaguliwa kujiunga na Vyuo vya Afya ngazi ya Stashahada.

(iv)Wanafunzi 52,934 wakiwemo wasichana 15,820 na wavulana

37,114 wamechaguliwa kujiunga kwenye kozi mbalimbali

zikiwemo za Kilimo, Ufugaji, Utawala, Biashara na zinginezo za

Stashahada katika Vyuo vya kati mbalimbali nchini.


Ndugu Wanahabari;

Muhula wa kwanza kwa wanafunzi wa Kidato cha Tano utaanza tarehe 14 Agosti,

2023. Hivyo, Wanafunzi wote waliopangwa kujiunga na Kidato cha Tano kwa

mwaka, 2023 wanapaswa kuanza kuripoti Shuleni kuanzia tarehe 13 Agosti,

2023. Siku ya mwisho ya kuripoti itakuwa tarehe 31 Agosti, 2023.

Fomu za maelezo ya mahitaji ya kujiunga na Kidato cha Tano (Joining Instructions)

kwa Shule zote za Kidato cha Tano zinapatikana kwenye tovuti ya kupitia

kiunganishi cha seleform.tamisemi.go.tz .

Ndugu Wanahabari;

Kwa wanafunzi waliopangwa kwenye Vyuo vya Elimu na Mafunzo ya Ufundi

watapokea maelekezo ya namna ya kujiunga kutoka Vyuo walivyopangwa.


Ndugu Wanahabari;

Uchaguzi wa wanafunzi wa kujiunga na Kidato cha Tano na Vyuo vya Elimu ya

Ufundi umefanyika kwa kuzingatia ufaulu na nafasi zilizopo katika Shule; hivyo,

hakutakuwa na fursa ya kufanya mabadiliko yoyote ya Shule kutokana na

ukosefu wa nafasi.


Ndugu Wanahabari;

Napenda kutumia fursa hii kuwapongeza walimu, wazazi na walezi wote kwa juhudi

walizozifanya katika ufundishaji na kuwezesha wanafunzi kufaulu vizuri. Naomba

wazazi/walezi wote tuendelee na moyo huu wa kusimamia na kufuatilia maendeleo

ya watoto wetu. Aidha, nawapongeza wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na

Kidato cha Tano, Vyuo vya Ualimu na Vyuo vya Elimu ya Ufundi. Napenda

kuchukua fursa hii, kuwahimiza kuendelea kufanya bidii katika kujifunza ili waweze

kufanikiwa kujiunga na mafunzo ya elimu ya juu baada ya kuhitimu Kidato cha Sita

na Vyuo vya Elimu na ya Ufundi.

Ninawashukuru Viongozi na Watendaji wa Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa

pamoja na Wananchi kwa ujumla kwa kushiriki kikamilifu kuimarisha miundombinu

ya Shule ikiwemo mabweni na majengo mengine yaliyowezesha Shule kupokea

wanafunzi wote waliopangwa Kujiunga na Kidato cha Tano.


Ndugu Wanahabari;

Nitumie pia fursa hii kutoa wito kwa Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na

Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha kuwa azma ya Serikali

ya kuwa na Shule za Sekondari za Kidato cha Tano katika kila Tarafa inatekelezwa

ili kuwezesha wanafunzi wote wanaofaulu Mtihani wa Kidato cha Nne kupata nafasi

ya kuendelea na masomo ya Kidato cha Tano na Sita. Upanuzi na ujenzi wqa Shule

Mpya za Kidato cha Tano na Sita uendelee kufanyika ikiwa ni pamoja na kuongeza

tahasusi za masomo ya sayansi. Mikoa ihakikishe inakuwa na tahasusi zote za

msingi katika Shule zake ili kuwapunguzia wazazi/walezi gharama za usafiri kwenda

Shule za mbali

Orodha ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na Kidato cha Tano, Vyuo vya

Ualimu na Vyuo vya Elimu ya Ufundi mwaka, 2023 inapatikana kwenye tovuti ya

Ofisi ya Rais -TAMISEMI ya selform.tamisemi.go.tz na Baraza la Taifa la Elimu ya

Mafunzo ya Ufundi ya www.nacte.go.tz.


Ndugu Wanahabari;

Pamoja na maelekezo haya, kwa mwanafunzi, mzazi/mlezi atakayekuwa na suala

linalohitaji maelekezo au ufafanuzi zaidi aende katika Ofisi za Elimu za Mikoa na

Halmashauri au apige simu kwenye namba ya Kituo cha Mawasiliano cha ORTAMISEMI kwa namba za simu 026 2160210 au 0735 160210.

Ahsanteni kwa kunisikiliza.

 

Mhe. Angellah J. Kariuki, (MB)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS -TAMISEMI.Â