Nairobi/Kenya. Wakati maandamano ya upinzani yakiendelea kwa Jumatatu ya pili nchini Kenya, kundi la watu limevamia shamba la Rais mstaafu, Uhuru Kenyatta wakakata miti na kuiba mifugo kadhaa wakiwemo mbuzi na kondoo.

Watu hao walionekana wakikata miti kwa kutumia misumeno ya umeme, kuiba mifugo kwa idadi isiyojulikana kisha kuchoma moto sehemu ya shamba hilo lililopo katika kaunti ndogo ya Ruiru.

Tovuti moja ya nchini humo iliripoti kuwa kundi hilo linadaiwa kuwatishia kuwakata mapanga waandishi wa habari na watu waliokuwa wakijaribu kurekodi tukio hilo.

Katika video za siri zilizovuja kwenye mtandao wa Twitter, ziliwaonyesha wavamizi wakiondoka na mifugo ikiwemo mbuzi na kondoo na wengine wakipakia katika magari yao.

Hakuna taarifa yoyote iliyotolewa ama na Serikali au familia ya Kenyatta aliyeondoka madarakani Septemba 13 mwaka jana na nafasi yake ikachukuliwa na William Ruto.

Tukio lingine ambalo lilishuhudiwa katika maandamano hayo yaliyoitishwa na Kiongozi wa Azimio la Umoja, Raila Odinga ni waandishi wa habari kutoka vyombo vya habari vya kitaifa na kimataifa kushambuliwa na kundi la watu wenye visu huko Kibra walipokuwa wakiripoti maandamano hayo.

Wengine kadhaa walijeruhiwa baada ya kundi hilo kufanya ghasia na kuyarushia magari ya wandishi mawe ndani ya eneo la Kibra.

Jase Ndungu, mwandishi wa habari wa runinga ya Citizen Kenya anayeripoti maandamano ya Kibra, alisema genge lililojihami na visu liliwavamia wanahabari hao na kuwalazimu kukimbia kuokoa maisha yao.

“Tulipokuwa tukiripoti maandamano yaliyokuwa yakiendelea, waandamanaji walikuwa wamewasha moto mkali na wakati tunachukua tukio hilo, ndipo tuliposhambuliwa,” alisema.

Kwa mujibu wa ripoti hizo, waandishi wa habari ambao hawakuweza kukimbia waliibiwa wakati wa tukio hilo na wengine kujeruhiwa.

Odinga aliyewahi kuwa waziri mkuu aliongoza maandamano hayo jana akiwa na viongozi wengine wa Azimio la Umoja jijini Nairobi, alihutubia katika maeneo kadhaa kwa dakika zisizozidi mbili.

Katika hotuba zake, Odinga alisikika akiwauliza wananchi “wangapi wanasema bei ya unga irudi chini?” na wananchi walijibu kwa kupiga kelele.


Sheria yapendekezwa

Wakati maandamano hayo yakiendelea wiki ya pili, Wizara ya Mambo ya Ndani kupitia taarifa kwa umma juzi ilipendekeza mabadiliko kwa sheria za usalama ambazo zinalenga kuongeza ugumu kwa watu kufanya maandamano nchini humo.

Katiba inawapa Wakenya haki ya kukusanyika, kuandamana na kupiga kura, lakini washiriki lazima wawe watulivu na bila silaha.

Mabadiliko yaliyopendekezwa na wizara yanalenga kupunguza idadi ya watu wanaofanya maandamano wakati wowote.

Katika mapendekezo hayo waandamanaji wanatakiwa kuwajibika kulipa fidia kwa wale watakaoathiriwa na shughuli za maandamano.

Katika mapendekezo ya mabadiliko hayo, wizara ya mambo ya ndani pia inataka kutengwa kwa maeneo ambayo watu wanaweza kukusanyika na kufanya maandamano.

“Haiwezekani kwa vyombo vya usalama kuruhusu umati wa watu kuzurura mitaani na vitongoji wapendavyo wakiwa wamebeba mawe na silaha nyingine za kukera ,huku wakiimba kaulimbiu za kisiasa na kutatiza shughuli za kila siku za wengine,” ilisema taarifa ya wizara hiyo.

Mabadiliko yaliyopendekezwa yamekosolewa na baadhi ya watu kama “kudharau misingi ya jamii iliyo wazi na ya kidemokrasia na kama sheria inayokiuka katiba”.


Polisi wayakabili

Katika hatua za kukabiliana na waandamanaji, polisi walirusha mabomu ya machozi kuwatawanya maandamano hayo..

Ulinzi ulikuwa mkali, huku polisi wa kutuliza ghasia wakiwa katika maeneo ya kimkakati jijini Nairobi na kushika doria mitaani, huku maduka mengi yakiwa yamefungwa na huduma za treni kutoka viunga vya mji mkuu hadi wilaya kuu ya biashara zilisitishwa.

Polisi walikabiliana na waandamanaji waliokuwa wakirusha mawe katika kitongoji kikubwa cha Nairobi cha Kibera, ambapo waandamanaji walichoma matairi, wakikaidi onyo la Inspekta Jenerali wa Polisi Japhet Koome alilolitoa Jumapili kwamba mikusanyiko hiyo “haramu” itapigwa marufuku.

Hali ilikuwa shwari kwingineko katika jiji hilo, huku kukiwa na polisi wengi katika vitongoji ambako maandamano yalikuwa yamefanyika wiki iliyopita.

Maandamano hayo ni ya pili baada ya yale ya Jumatatu juma lililopita dhidi ya Serikali kupinga kupanda kwa gharama za maisha.

Baadhi ya picha zilizosambaa zilionyesha uwezekano wa watu kadhaa kujeruhiwa na hata vifo.

Imeandaliwa na Victor Tullo kwa msaada wa mitandao ya kimataifaJOIN OUR SOCIAL MEDIA PLATFORMS FOR MORE UPDATES

👇👇👇👇👇👇 


TAP HERE TO JOIN OUR TELEGRAM CHANNEL (New)💥

TAP HERE TO VISIT OUR WEBSITE

TAP HERE TO DOWNLOAD OUR APP (GOOGLE PLAY STORE)