Muktasari:

  • Bao la Clatous Chama alilofunga dakika ya 45 limetosha kuipa Simba ushindi katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Vipers katika uwanja wa Mkapa.

Dar es Salaam. Klabu ya Simba imeibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Vipers ya Uganda katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika kwenye hatua ya makundi iliyochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa ikijiongezea matumaini ya kutinga robo fainali.

Chama alifunga bao hilo akitumia vizuri pasi ya Moses Phiri ambaye alimpenyezea na yeye kuweka wavuni.

Ushindi huo unaifanya Simba kufikisha pointi sita na mabao mawili ikishika nafasi ya pili katika kundi C huku nafasi ya kwanza ikiwa ni Raja Casablanca ikiwa na pointi 12 baada ya kuichapa Horoya mabao 3-1 leo.

Simba imeendeleza ubabe kwa Vipers kwenye mechi mbili mfululizo ikishinda nyumbani na ugenini katika hatua hii ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika.

Katika mchezo wa kwanza nchini Uganda, Simba ilishinda 1-0 bao likifungwa na Henoc Inonga na kwenye mchezo wa leo uwanja wa nyumbani imeshinda tena 1-0.

Nafasi ya tatu ipo Horoya ikiwa na pointi nne huku Vipers ikishika mkia ikiwa na pointi moja pekee.

Simba itakuwa barua kingine cha kusaka pointi tatu mbele ya Horoya Machi 18 katika uwanja wa Mkapa huku Vipers ikiisubiri Raja Casablanca nchini Uganda.