Muktasari:

  • Raja ndio kinara wa Kundi C ikiwa na pointi 13, huku Simba ikifuata nyuma yake ikikusanya pointi tisa na zote zikiwa zimeshafuzu robo fainali ya michuano hiyo na mechi hiyo ya mwisho ya kufungia hesabu itakuwa ni ya kutafuta heshima ikiziangatiwa mchezo wa awali Wekundu walilala mabao 3-0.

Dar es Saalam. Simba inarejea jana mazoezini kujifua kwa ajili ya mechi ya mwisho ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika ugenini Morocco dhidi ya Raja Casablanca, itakayopigwa April Mosi jijini Casablanca, huku benchi la ufundi la chama hilo likiwa limepanga kuwasapraizi waarabu hao nyumbani kwao.

Raja ndio kinara wa Kundi C ikiwa na pointi 13, huku Simba ikifuata nyuma yake ikikusanya pointi tisa na zote zikiwa zimeshafuzu robo fainali ya michuano hiyo na mechi hiyo ya mwisho ya kufungia hesabu itakuwa ni ya kutafuta heshima ikiziangatiwa mchezo wa awali Wekundu walilala mabao 3-0.

Kutokana na kubaini kuwa hiyo ni mechi ya heshima na ya kulipa kisasi kutokana na kipigo hicho cha aibu ilichopewa timu yake nyumbani, Kocha Mkuu wa Simba Roberto Oliveira 'Robertinho' aliliambia Mwanaspoti ameandaa mkakati tofauti wa kucheza mechi na Raja kutokana na wachezaji wake wengi wa kikosi cha kwanza kuwa kwenye timu zao za taifa kwa sasa.

Wachezaji hao ni Makipa Aishi Manula na Beno Kakolanya, kiungo Mzamiru Yassin (Tanzania), Clatous Chama (Zambia), Henock Ingonga (DR Congo), Peter Banda (Malawi), Pape Sakho (Senegal) na Saidi Ntibanzonkiza (Burundi).

"Mechi ijayo itakuwa tofauti kidogo, tutacheza kimkakati na kuhakikisha tunapata matokeo mazuri licha ni mchezo mgumu kwetu. Kutokana na wachezaji wengi wa kuwa katika majukumu ya timu zao za taifa kunaweza kuwa na mabadiliko pia kwenye kikosi," alisema Robertinho na kuongeza;

"Tuna timu yenye wachezaji wengi hivyo tutawapa nafasi watakaokuwa tayari na naamini watafanya vizuri."
Robertinho alisema moja ya sapraizi aliyowaandalia Raja ni kuwatumiza zaidi wachezaji ambao hawatumiki mara kwa mara, huku akiwataja Kennedy Juma, Erasto Nyoni ana mipango nao katika pambano hilo la kukamilisha ratiba ya makundi ya michuano hiyo ya CAF.

katika hatua nyingine, Robertinho alisema wakati msimu unakaribia kumalizika, tayari ameaanza kufanya uchambuzi wa kikosi chake na kupiga hesabu za kuongeza mastaa wapya huku akimtaja Hassan Dilunga aliyepona na kurejea mazoezini SImba licha ya kuwa hayupo kwenye usajili wa msimu huu.
"Nafuatilia kwa karibu wachezaji wote wa Simba na wale wa timu nyingine na mwisho wa msimu nitatoa ripoti kwa uongozi itakayokuwa imejumuisha kila kitu.

Dilunga nimemuona lakini nahitaji muda zaidi kwani amekuja kipindi ambacho mara nyingi tunafanya mazoezi kwa ajili ya mechi husika, tutakuwa naye na mwisho itajulikana nini tutaamua." alisema Robertinho mwenye malengo ya kuipa ubingwa wa Afrika Simba.


MECHI ZIJAZO SIMBA
Aprili 01, 2023
v Raja (CAF-ugenini)

Aprili 07, 2023
v Ihefu (ASFC-nyumbani)

Aprili 10, 2023
v Ihefu (Ligi-ugenini)

Aprili 16, 2023
v Simba (Ligi-nyumbani)