Mwanza. Uamuzi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino cha Tanzania (Saut) kufuta shahada za wahitimu 162 kutoka Chuo cha Tiba cha Mtakatifu Francis, Ifakara umeibua mjadala huku wadau wa elimu wakigawanyika.

Licha ya kukiri kuwa seneti ndicho chombo chenye mamlaka na uamuzi wa mwisho wa masuala yote ya vyuo vikuu, baadhi ya wadau wameshauri busara na ubinadamu utumike kwa kufuta taarifa za matokeo badala ya shahada.

Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa jana na kusainiwa na Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu Saut, Profesa Costa Mahalu, uamuzi wa kufuta shahada hizo umefikiwa baada ya wahitimu hao waliohitimu kati ya mwaka 2015 hadi 2019 kukaidi agizo la kurejesha taarifa za matokeo zilizotolewa bila idhini ya seneti.

Waliofutiwa shahada ni kati ya wahitimu zaidi ya 300 waliotakiwa kurejesha taarifa zao za matokeo, ambapo baadhi walitii agizo na 162 kukaidi.

Chuo cha Tiba cha Mtakatifu Francis, Ifakara kiko chini ya Saut.

Akizungumza na Mwananchi kwa simu jana, Profesa Mahalu alisema uamuzi huo uliozingatia kifungu cha 47(1) na (2) cha Sheria ya Vyuo Vikuu namba 7 ya mwaka 2005 ikisomwa pamoja na kifungu cha 6(3)(ii), 7, 8 na kanuni ya 29(1) ya charter ya Saut ulifikiwa na kikao cha dharura cha Seneti kilichoketi Machi 25, 2023.

“Wahitimu wote wanapaswa kufahamu kuwa taarifa za matokeo, vyeti na shahada ni mali ya chuo na lazima zipitishwe na Seneti. Transcripts zilizofutwa hazikupitishwa na seneti. Sasa ni wajibu wao kuzirejesha ili wapewe mpya zilizoidhinishwa,” alisema Profesa Mahalu

Aliongeza, “sasa ni jukumu na wajibu wa wahitimu hao kutii agizo la seneti kwa kurejesha taarifa za matokeo zilizoidhinishwa kwa mujibu wa sheria.”

Alisema agizo la kurejesha taarifa hizo halikuwa na madhara kwa wahitimu wala shahada zao, bali kilichotakiwa kurekebishwa ni alama za ufaulu kulingana na mfumo mpya uliotolewa na Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) mwaka 2015

“Kilichotakiwa kufanyika ni kubadilisha transcripts zilizotolewa kimakosa huku wahitimu wakibaki na hati zao na transcripts za zamani ambazo zina grading system iliyopitishwa na Senate ya Saut,” alisema Profesa Mahalu.

Kwa mujibu wa Profesa Mahalu, baadhi ya viongozi wa Chuo cha Tiba cha Mtakatifu Francis waliohusika kutoa taarifa za matokeo ya wahitimu bila kuidhinishwa na seneti tayari wamewajibika kwa kuachia nafasi zao.

Akizungunzia madhara kwa wahitimu waliofutiwa shahada, hasa waliojiendeleza kielimu wakitumia shahada zilizofutwa, Profesa Mahalu alisema Saut haiwezi kuviamulia vyuo vilivyowatunuku shahada hizo nini cha kufanya.

“Hilo litawahusu wahitimu na vyuo walivyohutimu na kutunukiwa shahada zingine zilizotokana na zilizofutwa,” alisema.

Hata hivyo, baadhi ya waathirika baadhi yao wakiwa wameajiri, waliiambia Mwananchi kuwa wanaamini wana haki kisheria.

“Tulipewa nakala na vyeti vilivyotiwa saini na seneti ya chuo kikuu na baadhi yetu tulivitumia kuombea kazi, hii si haki kwetu hata kidogo na mimi binafsi nitakata rufaa kisheria,” alieleza mmoja wa wahitimu hao.

Mwingine aliyetaka jina lake lihifadhiwe, alikiri kupokea notisi mara tatu iliyomtaka arejeshe nakala hiyo chuoni, lakini alisita kutekeleza hilo.

Mhitimu mwingine aliyejitaja kama Sophia, alisema hakuona matangazo ya kutakiwa kwa nakala hizo kwenye magazeti, alichokiona ni picha ya kipande cha tangazo la kuvuliwa shahada ikiwa na jina lake.

Akizungumzia suala hilo, mshauri wa masuala ya elimu, Dk Wilberforce Meena alisema, “binafsi naona si sahihi kufuta shahada za wahitimu iwapo walifanya na kufaulu mitihani yao bila udanganyifu; nadhani njia sahihi ingekuwa kuwafutia taarifa za matokeo. Mdau wa Elimu, Avemaria Semakafu alisema kisheria, seneti ndiyo inaidhinisha matokeo ya wahitimu wa vyuo vikuu, hivyo ni kosa iwapo taarifa za matokeo zilitolewa na uongozi wa chuo bila idhini ya seneti.

“Hata hivyo, kosa hilo si la wanafunzi, bali ni la kiutawala kwa uongozi wa chuo uliotoa taarifa ya matokeo yasiyoidhinishwa na seneti,” alisema Semakafu aliyewahi kuwa naibu katibu mkuu Wizara ya Elimu.


Ilivyoanza

Sakata lilianza mwaka 2015 baada ya TCU kutoa mwongozo mpya wa upangaji matokeo kwa vyuo vikuu unaoelekeza alama A kutolewa kuanzia ufaulu wa asilimia 70 hadi 100.

Profesa Mahalu alisema wakati huo kuwa maelekezo hayo yalikinzana na viwango vya ufaulu vya Saut iliyokuwa inaelekeza alama A kutolewa kwa ufaulu unaoanzia asilimia 80 hadi 100 lakini chuo husika kikatumia mfumo tofauti na maelekezo, hivyo kukilazimu uongozi wa Saut kuitisha upya fomu za matokeo ili kutoa nyingine.


JOIN OUR SOCIAL MEDIA PLATFORMS FOR MORE UPDATES

👇👇👇👇👇👇 






TAP HERE TO JOIN OUR TELEGRAM CHANNEL (New)💥

TAP HERE TO VISIT OUR WEBSITE

TAP HERE TO DOWNLOAD OUR APP (GOOGLE PLAY STORE)