Wakati ligi mbalimbali zikielekea ukingoni, kuna rundo la wachezaji wapo nje ya uwanja wakiuguza majeraha waliyoyapata katika majukumu yao msimu huu na wengine hawajatumikia kabisa hata  mchezo hata mmoja tangu msimu uanze.
Kinachoshangaza ni kwamba baadhi ya mastaa wamekuwa majeruhi wa muda mrefu, kiasi cha kuzua hisia tofauti, lakini Mwananchi kwa kushirikiana na baadhi ya madaktari wa timu na wachezaji wakongwe wa soka wamebaini baadhi ya mambo yanayochangia majeruhi hao kuchelewa kupona.
Wataalamu hao wamebainisha mambo yanayochangia kwa wachezaji wa ligi zetu kutopona haraka majeraha yao licha ya kupewa muda fulani wa matazamio ya kupona na kurejea uwanjani kulingana na aina ya majeraha wanayokuwa nayo.
Moja ya tatizo kubwa ni imani za kishirikina ambazo zimefanya mastaa wengi kukacha kuwahi kupatiwa matibabu kitaalamu na kujiumiza zaidi, lakini hata vitendo vya kuendekeza ngono, aina ya vyakula na kukosekana matibabu sahihi ni mambo yanayowadhuru zaidi. 

MTIHANI MKUBWA
Hakuna ubishi kwamba majeraha yamewafanya wachezaji wengi kushindwa kurejea kwenye ubora waliokuwa nao awali kabla ya kuumia na wengine wamejikuta wakipoteza namba na wengine wakishindwa kurudi kabisa uwanjani na kupoteza ndoto zao kwenye soka.
Kuna sababu nyingi ambazo zinasababisha mchezaji kutopona haraka jeraha alilopata ambapo wataalamu hao leo wanafunguka kiini cha tatizo hilo linalosumbua watu wengi.
Daktari wa timu ya Tanzania Prisons, Kilulu Masunga anasema moja ya kuchelewa kwa jeraha kupona inategemeana na aina ya jeraha alilonalo mchezaji.
Anasema kuna utofauti kwa mchezaji anayepata jeraha kwa ndani na yule anayepata jeraha la nje mfano mtu aliyevunjika mfupa ukatoka hadi nje 'open fracture' atachukua muda mrefu ukilinganisha na yule aliyevunjika kawaida 'closed fracture' au tatizo la misuli na kuchanika nyama.
Aliyekuwa daktari wa Yanga, Shecky Mngazija anasema kuna wakati makadirio yanaweza yasiwe sahihi, umri unachangia mtu kupona haraka au kuchelewa, kugundua ugonjwa tofauti na uliopo pamoja na ukosefu wa lishe bora.
Daktari wa timu ya Polisi Tanzania, Richard Yomba anasema mchezaji moja ya vitu ambavyo vinaweza kusababisha mchezaji kupona haraka ni pamoja na utumiaji sahihi wa dawa, muda sahihi na dozi sahihi.
Kwa upande wa Dk Mwanandi Mwankemwa, daktari wa timu ya Azam anasema jeraha lolote linakuwa na muda wake wa kupona mfano mtu aliyevunjika mkono huweza kuchukua wiki nne kutokana na mzunguko wa damu tofauti na aliyevunjika mguu itachukua wiki nane hadi tisa.
Anasema mtu anapopata jeraha anatakiwa kupata matibabu yaliyosahihi, lishe bora na mazoezi maalumu kutoka kwa wataalamu na akikosa vitu hivyo atachelewa kupona na hata akipona tatizo linaweza kujirudia.

UDANGANYIFU WA UMRI
Dk Samwel Shita anasema uponaji wa jeraha, hutegemeana pia na umri wa mchezaji, mchezaji mwenye umri mdogo uponyaji wake unakuwa haraka kuliko mwenye umri mkubwa.
"Mtu mwenye tatizo la mifupa umri ndio unaangaliwa zaidi, hivyo unapodanganya itachelewesha uponyaji wako kulingana na makadirio ambayo yamewekwa na wataalumu.
"Mwisho wa ukuaji wa mifupa huwa kwa mtu mwenye miaka 25, ukidanganya hata uponyaji wako unachelewa sababu daktari anaweza akakupa matibabu na muda wa makadirio akijua upo chini ya miaka 25 kumbe una miaka 30.
Dk Masunga anasema suala la umri ni tatizo kubwa sana kutokana na hali ya maisha yetu na wachezaji wengi wanaonekana kudanganya umri wao.
"Unamsajili mchezaji U20 lakini ukweli ni kwamba hana umri huo na hapa inawaathiri zaidi wale wanaopata tatizo la mfupa sababu kila umri unavyoongezeka na mfupa pia hukomaa.
Dk Yomba anasema hilo lipo wazi kwa wachezaji wengi kuficha umri lakini anapopata tatizo ndio utajua kwamba alidanganya umri wake na sasa anateseka.


NGONO NI TATIZO
Dk Shita anasema kitendo cha kufanya ngono, hutumika nguvu nyingi hivyo mchezaji anapopata tatizo hushauriwa kupumzika ili nguvu nyingi ibaki katika kuunga jeraha.
Dk Masunga anasema utimamu wa mwili 'fitness' ya mchezaji inaweza ikaharibiwa kama atajihusisha na tendo hilo, japo halijathibitika kisayansi ndio maana hata kukiwa na mchezo mkubwa wachezaji hubanwa wasitoke maana wakihofiwa kushuka kiwango.
"Hivi vitu tumevikuta na vinaendelea kuwa stori na vinaingia kwenye jamii, lakini binafsi sioni kama ina uhusiano wowote vitu hivyo katika soka."
Dk Mngazija anasema kutofuata masharti ya kitabibu ni kosa kubwa ambalo wengi wanalifanya maana anapomwambia mchezaji asifanye mapenzi ina maana yake.
"Kwanza unatakiwa kujua kufanya mapenzi ni starehe sasa kama mtu anaumwa anastarehe vipi wakati yeye ni mgonjwa, ndio maana inashauriwa kwa muda huo asijihusishe sababu atatumia nguvu nyingi katika tendo hilo.
Dk Yomba anasema watu wanachanganya sana mambo kwenye hili jambo na wachezaji wanakatazwa sababu wana tabia ya kutoka nje ya mtu wake (mke), hivyo anapotoka nje ya ndoa anafanya kama anakomoa ili kwenda na mtindo kumbe anajitonesha jeraha.
"Ishu ya mapenzi wenzetu Ulaya wanaishinda sababu hawana mambo mengi, sisi tuna mambo mengi yaani mchezaji akiwa na mke wake hata kama siku moja kabla ya mchezo anaweza kulala naye na kesho akacheza vizuri.
Dk Mwankemwa anasema hii ni dhana potofu ambayo watu wanakuwa nayo sababu suala la mapenzi ni sehemu ya maisha, hivyo haamini kuhusu hilo, japo kitaalamu majeruhi ushauri kuacha kwa muda.

USHIRIKINA
Dk Shita anasema ushirikina ni imani potofu ambayo inachangiwa zaidi na suala la kisaikolojia kwa mchezaji baada ya kuumia anakuwa na hofu ya ushirikina kutokana na tatizo alilolipata.
"Akikutana na watu ambao nao watamtishia na imani za kishirikina, lazima imuathiri kisaikolojia na anaweza akaamini kuwa amerogwa na kutoamini matibabu ya kitaalamu na kukimbilia anakojua yeye kupata ufumbuzi na hivyo kujiweka kwenye hatari ya kujidhuru zaidi kuliko kulitibu tatizo," anasema, huku Dk Masunga yeye anasema kuna majeraha mchezaji anatakiwa akae nje ya uwanja kwa muda wa miezi mitatu hadi minne, lakini akiangalia soka ndio inaendesha maisha yake anaanza kuhangaika na kwenda kwa waganga wa kienyeji (sangoma), ili kupata matibabu pamoja na kwamba ameshatumia dawa za daktari.
"Changamoto hii ni kubwa na nimewahi kukutana nayo sababu mpira unajumuisha vitu vingi sana na kuumia ni vitu vya kawaida maana inategemeana mwenzako amekugonga eneo gani au ulianguka vibaya," anafafanua Dk Masunga na kuongeza kwa kusema kuwa, wachezaji wengi wanakuwa na imani za kishirikina na kila tukio wanalokumbana nalo hulihusisha na mambo ya kiimani za kishirikina hata kama unamweleza tatizo lake la kawaida na linatibika na kupona vyema mapema.
"Mchezaji anapokuwa kwenye kiwango bora kwa michezo miwili au mitatu halafu akaumia hawezi kuamini kwamba lile jeraha kaumia katika mazingira ya kawaida uwanjani, hivyo hata daktari unapokaa inakubidi uanze kutumia saikolojia kumwelezea," anasema.
Anaongeza baada ya siku chache anapokuwa kwenye matibabu, huku akiona wenzake wakiendelea na mazoezi anaona amechezewa na kuwakimbia akiamini amechezewa.
"Hili suala la kiimani za kishirikina limetawala sana kwenye soka letu na nimekutana nalo mara nyingi unamtibu mchezaji halafu unampa muda wa mapumziko, lakini siku unamkagua unakuta tayari ana chale ameshachanja halafu anakuambia tayari nimeshapona, hivyo ni vitu ambavyo tunakutana navyo sana.
Dk Mngazija anasema inapofikia hatua mchezaji kuanza kufikiria suala la dawa mbadala inatokana na daktari kwanza namna alivyomuandaa kisaikolojia mchezaji wake kutokana na tatizo alilokua nalo.
"Binafsi sijawahi kukutana na mchezaji wa aina hiyo, labda kama amelifanya na sikugundua lakini kama daktari unapaswa kumweka wazi kwamba tatizo lako halihusiani na mambo ya kishirikina, hivyo inategemeana na maelezo yako kwake na yasipojitosheleza na kumweka katika imani halisi lazima aende pembeni."
Dk Yomba anasema hata (jina kapuni), nilishawahi kumwambia tatizo lako ni la hospitali lakini akanitoroka na kuwaomba ruhusa viongozi kwamba anakwenda kujitibia, akachanjwa kisha akarudi na tatizo likajirudia.
"Sawa kuna tiba asili na hospitali, lakini sipendi kuamini sana sababu mwisho wa siku wanakwenda kuishia pabaya sana tena kwa kufanyiwa upasuaji mfano (jina kapuni) amecheza akiwa na tatizo la goti muda mrefu sana."
Dk Mwankemwa anasema mchezaji kuamini amerogwa amewahi kukutana nalo akiwa timu ya taifa, Taifa Stars anamtaja mchezaji (jina kapuni) aliyekuwa mchezaji wa (timu moja) alivunjika mguu na kushauri kufanyiwa upasuaji.
"Alikataa akatuambia yeye ana mtaalamu wake huko anakokaa na anaunga mifupa kwa njia ya asili, basi akaachiwa kambini na kwenda kwenye matibabu lakini hakuweza kupona na hiyo ndio ilikuwa mwisho wa maisha yake ya soka," anasema Dk Mwankemwa na kuongeza;
"Kuna wakati viongozi wa timu moja hapa nchini waliniomba nimfanyie mpango aende Nairobi akatibiwe, lakini sababu zile imani zilishamjenga kwamba atapona kwa dawa za asili hakuweza kukubali na tangu hapo sijamuona tena uwanjani hivyo vitu hivi vipo."
Anaongeza kwa kuwashauri wachezaji kufuata maelezo ya wataalam wao hasa wanapopata tatizo kuliko kukimbilia matibabu ambayo hawana uhakika wa kupona.
Yapo madai kuwa kuna baadhi ya wachezaji ambao wamekuwa wakikimbilia vijijini kwao kila wapatapo matatizo ya majeraha kwa kuamini wamerogwa ndipo wakijiridhisha hufuata matibabu ya kitaalamu hospitalini na kupona kabisa na kurejea uwanjani, pia inaelezwa hata wachezaji kutoka nje ya nchi wanapoumia wanakimbilia kutibiwa nchini kwao.
Hivi karibuni nyota wa zamani wa Ruvu Shooting aliyewahi kukipiga Yanga, Kagera Sugar na Lipuli, Ally Mtoni 'Sonso', alifariki dunia, ilibainika kucheleweshwa kupata matibabu sahihi hospitalini ilichangia mauti yake.
Msemaji wa Ruvu, Masau Bwire alinukuliwa akisema Sonso aligomea matibabu ya hospitalini akiungwa mkono na ndugu zake na kufanya ashindwe kupona kwa haraka kabla ya mauti kumkumba Februari mwaka jana.

MWENENDO WA MAISHA
Mwenendo na mitindo mibaya ya mchezaji muda mwingine husababisha ucheleweshwaji wa kupona kwa jeraha lake mfano ili jeraha liweze kuunga lazima kushikamana na ushauri wa daktari ikiwamo kupumzika, kutotumia kiungo hicho kabla ya muda ambao daktari amepanga.
"Mfano daktari akakuambia utapumzika kwa wiki mbili baada ya hapo ndio utaanza kukanyagia, sasa utakuta mchezaji anaanza kukanyaga kabla ya muda aliopangiwa, hivyo jeraha linakuwa limejitonesha na kuongezeka ukubwa.
JOIN OUR SOCIAL MEDIA PLATFORMS FOR MORE UPDATES

JOIN OUR WHATSAPP GROUP  

👇👇👇👇👇👇 


TAP HERE TO JOIN OUR TELEGRAM CHANNEL

TAP HERE TO VISIT OUR WEBSITE

TAP HERE TO DOWNLOAD OUR APP (GOOGLE PLAY STORE)


Please leave your comment on our service.......................