Muktasari:

  • Kikundi cha wanawake kilichopata mkopo wa halmashauri wa Sh130 milioni, kimenunua gari aina ya tata watakalotumia kuzombea taka ili kujiongezea kipato.

Kiteto. Kikundi cha wanawake cha Kiteto Sanitation, kimepewa mkoapo wa kununulia gari la kusomba taka la thamani ya Sh130 milioni kwa ajili ya mji wa Kibaya.

Akikabidhi hundi ya Sh130 milioni kwa kikundi hicho leo Machi 9, 2023, mwakilishi wa Mkuu wa wilaya ya Kiteto, Kaimu Ofisa Tawala wa wilaya hiyo, Fadhili Alexander amesema, kwa mara ya kwanza halmashauri hiyo imetoa fedha kwa vikundi vyenye sifa.

"Tunajua Sh2 milioni ambazo hutolewa na halmashauri kwa kila kikundi huwa zinaleta vurugu kwenye vikundi sasa hizi Sh130 milioni ni nyingi hivyo mnapaswa kuwa makini nazo kwani mnatakiwa kufanya marejesho," alisema Alexander.

Akizungumzia mkopo huo, Mbunge wa Jimbo la Kiteto, Edward Lekaita amesema Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imejipanga kutoa kipaumbele kwa wananchi hasa wanawake.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, John Nchimbi amesema fedha hizo zitatumika kununulia gari maalumu la kusombea taka katika mji wa Kibaya.

“Gari hili ni aina ya Tata ambalo pia litatumika kwa shughuli mbalimbali za kijamii lakini zitanufaisha zaidi kikundi hicho ambacho awali kililazimika kukodi magari ya kusomba taka," amesema Nchimbi

Kwa upande wa wanufaika wa kikundi hicho wameshukuru halmashauri kuwapa kiasi hicho cha fedha kwa wakati mmoja na judai kitasaidia haswa kipindi hiki ambacho awali walilazimika kukodi magari ya kubebea taka

"Tunashukuru Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto kwa kuona haja ya kutupatia fedha nyingi kiasi hiki mil 130 ambazo tutanunua gari kurahisisha shughuli zetu za usafi mji wa Kibaya," amesema Zena Pambamoto.

Naye Sangoma Mohamed amesema watafanya kazi bega kwa bega na wataalam ili kuhakikisha gari hilo linapata matunzo.