Muktasari:

  • Mabeki wa Simba, Shomari Kapombe Na Mohamed Hussein 'Tshabalala' wameongezwa kwenye kikosi cha timu ya taifa 'Taifa Stars' kinachojiandaa na mchezo wa marudiano wa kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) dhidi ya Uganda.

Dar es Saalam. Mabeki wa Simba, Shomari Kapombe Na Mohamed Hussein 'Tshabalala' wameongezwa kwenye kikosi cha timu ya taifa 'Taifa Stars' kinachojiandaa na mchezo wa marudiano wa kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) dhidi ya Uganda.

Hayo yamesemwa na Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania, Wallace Karia wakati akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam.

"Maneno yalikuwa mengi sana baada ya uteuzi uliofanyika mwanzoni lakini tumeona matunda yake, kuongezwa kwa Kapombe na 'Tshabalala' ni pendekezo la Kocha Mkuu, Adel Amroache na tayari wamejiunga kambini na wenzao," amesema Karia.

Taifa Stars ilishinda mchezo wake wa kwanza ugenini dhidi ya Uganda Cranes uliochezwa Machi 24, mwaka huu katika Uwanja wa Suez Canal nchini Misri kwa bao pekee la Simon Msuva.

Mchezo wa marudiano baina ya Stars dhidi ya Cranes unatarajia kuchezwa Jumanne Machi 28, mwaka huu katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Stars ipo nafasi ya pili kwenye kundi F na pointi nne, nyuma ya vinara Algeria walioshinda mechi zote tatu huku Niger ikishika nafasi ya tatu na pointi mbili na Uganda ikiburuza mkia na pointi moja.