MPANGO KAZI HUU UNALETWA KWENU NA MaxMalick : 

  • Historia fupi ya kabila la Wameru, 
  • Kiini (lugha na utambulisho wa kabila la Wameru) 
     (a). Utambulisho katika majina. 
i. Majina ya watu. - Majina ya ukoo, - Majina ya rika, - Majina ya asili. 
ii. Majina ya vyakula.
iii. Majina ya mazao ya chakula. 

        (b). Utambulisho katika usemaji. 
i. Lafudhi, 
ii. Kiimbo, 
iii. Wakaa, 
iv. Mkazo, na 
v. Ufupishaji wa maneno. 
vi. Udondoshaji na ukiushi. 
  • Marejeo. 


HISTORIA FUPI YA KABILA LA WAMERU. 

Lugha ya Kimeru ni miongoni mwa lugha za kibantu inayozungumzwa nchini Tanzania na jamii ya wameru (wa-rwa). 
Kabila hili la wameru (warwa/ki-rwa) linatokana na wachaga wa machame waliohamia maeneo ya Meru-Arusha na kuchangamana na waarusha na hivyo lafudhi ya kimachame kuweza kubadilika kidogo kutokana na mwingiliano huo na kutengeneza au kuzaa lugha mpya (lafudhi mpya) ikijulikana kama KIMERU kwa sasa. 
Kutokana na maingiliano na maathiriano haya, kwa sehemu kubwa wameru na wamachame kinachowatofautisha ni lafudhi tu kwani kwa sehemu kubwa maneno wanayoyatumia huwa ni sawa na wanaelewana. 
Kutokana na hali hii, baadhi ya majina ya ukoo na ya kisifa kwa wameru na wamachame yanafanana. Mfano wa majina ya ukoo ni pamoja na Ndosi na Urio, na majina ya kisifa ni pamoja na Urasa, Swai, Kimaro, Kweka, na Masawe. 
Pamoja na maingiliano haya bado kabila la kimeru linaweza kujibainisha miongoni mwa watumiaji wa lugha ya Kiswahili nchini Tanzania hasa katika majina, vyakula, na hata namna ya kuzungumza, hii ni kwa sababu lugha ni kipengele muhimu katika utambulisho wa mtu. Sababu zifuatazo zinzthibitisha dai hili: 



 1. UTAMBULISHO KATIKA MAJINA. 

 (a). MAJINA YA WATU.

 i. MAJINA YA UKOO. 
Jamii za wameru huweza kutambuliwa kwa majina ya koo mbalimbali wanazotokana nazo. Baadhi ya koo hizo ni pamoja na: Mbise, Nnko, Pallangyo, Kaaya, Nassari, Sumari, Kitomari, Sarakikya, Akyoo, Sikawa, Nyiti, na Nanyaro. 2 Haya ni baadhi ya majina ya koo za kimeru ambapo yanapotajwa ama kutumiwa basi wahusika moja kwa moja wanaweza kutambuliwa kuwa ni wameru. 

ii. MAJINA YA RIKA. 
Neno rika hurejelea jamii au kundi la watu ambao walizaliwa katika kipindi kimoja na umri wao kwa hakika hautofautini sana (tofauti ya miaka 14 toka rika moja kwenda rika lingine). Majina ya asili kwa wameru hutolewa kwa mtu kutokana na rika lake. Mfano; Sitimu, Kisali, Seuri, Rekoti,Mangusha, na Kilowiyo. Haya ni majina yanayotumiwa na wameru na yanapotajwa yanayowatambulisha wameru hasa hapa nchini Tanzania. 

iii. MAJINA YA ASILI.
Kwa mujibu wa Tabouret-Keller na Le Page (1986), majina ya asili yanayotumiwa katika mawasiliano ya jamii hutolewa katika lugha za asili za jamii husika. Majina hayo hubeba maana mbalimbali zinazohusu utamaduni wa jamii hizo na mazingira yake. 
Hii humaanisha kuwa maana ya majina hayo hueleweka kwa wanajamii wenyewe kwakuwa wao ni sehemu ya utamaduni wa jamii hizo na mazingira yake. Kwa jamii za wameru majina ya asili yamekuwa sehemu muhimu ya utambulisho wao nchini Tanzania. Inaaminika kuwa majina haya yalianza kutumika kabla ya uvamizi wa watu weupe (wakoloni) katika bara la Afrika. 
Majina haya yana pande mbili yaani majina yanayowatambulisha wanaume na yanayowatambulisha
 wanawake kama inavyobainishwa katika mifano ifuatayo: 3Majina haya yanatumiwa na wakristo katika jamii hii ya kimeru na yanapotajwa ni rahisi mtu kugundua kuwa mwenye jina ni mmeru.  


(b) MAJINA YA VYAKULA. 
Kuna baadhi ya majina ya vyakula ambapo yanapotajwa hurejelea kuitambulisha jamii ya wameru kwani huwa ni sehemu ya utamaduni wao na pia majina yanayotumiwa aghalabu huwa ni ya jamii hiyo tu. 
Mfano; 
1. Nswa (loshoro). Hiki ni chakula cha aina ya makande yaliyochanganywa na ndizi ng’ombe na kasha kupekechwa na maziwa. Chakula hiki hakiwekewi kiungo chochote. Hutumiwa na watu wote. 

2. Kitalolo. Hiki ni chakula kwa ajili ya wanawake tu. Huandaliwa kwa mahindi, maharage na mboga za majani (mnafu tu). Chakula hiki pia hakiwekewi kiungo chochote. 

3. Usomu. Ni chakula cha kawaida ambacho ni cha maharage na mahindi kidogo kisha husongwa ili kuleta mchanganyiko mzuri. 

4. Uru. Hiki huwa ni chakula maalum kwa ajili ya mzazi (mama aliye jifungua). Chakula hiki huwa na mchanganyiko wa uji wa ulezi uliochanganywa na mafuta ya ng’ombe au kondoo na kisha kutiwa maziwa. Aidha, majina hayo yaliyotajwa hapo juu; kitalolo, nswa, usomu, na uru, yanapotajwa mtu huweza kubaini kuwa ni vyakula vya jamii ya kimeru na kurahisisha utambulisho wa mtu. 


(c). MAJINA YA MAZAO YA CHAKULA. 
Kuna majina yanayotumika kurejelea baadhi ya mazao ambapo majina hayo hutumiwa na jamii za wameru na hivyo yanapotajwa ni rahisi kugundua kuwa huenda muhusika ni ama ni mmeru au mwenyeji wa jamiia hiyo. 
Mfano; 
i. Meemba mahindi,
ii. Maruumi magimbi, 
iii. Maarakyi maharage, 
iv. fisoiya viazi, na 
v. Maruu ndizi. 


UTAMBULISHO KATIKA USEMAJI.

Katika suala la kubaini utambulisho wa wameru kwa njia ya usemaji wao, tutajikita katika kuangalia yafuatayo: Lafudhi, Kiimbo, Wakaa, Mkazo, na Ufupishaji wa maneno. 

i. LAFUDHI. 
 Kwa mujibu wa Massamba, Kihore, na Msajila (2004), lafudhi ni sifa ya kimasikizi (inayohusiana na kusikika kwa sauti wakati wa kutamka) ya matamshi ya mtu binafsi ambayo humpa msemaji utambulisho fulani ama kijamii au kieneo (kijiografia). Kwa namna nyingine lafudhi hutokana na athari ya mazingira ya mtu kijamii au kijiografia. 

Kwa upande wa wameru, kama ilivyo kwa makabila mengi nchini Tanzania, Kiswahili kwao ni lugha ya pili. Hii imewasababishia athari inayokana na lugha mama katika utamkaji wa baadhi ya sauti za lugha ya Kiswahili kama mifano ifuatayo inavyobaini:

 Mfano: Wameru huchanganya matamshi ya; 
 (a). sauti /s/ na /z/, Zamani hutamkwa Samani, 
 (b). sauti /v/ na /f/, Vaa nguo hutamkwa Faa nguo, 
 (c). sauti /ð/ (dh) na /s/. 
 Fedha hutamkwa Fesa. Matamshi yenye aina ya lafudhi zilizobainishwa hapo juu yanaposikika katika lugha ya Kiswahili, ni rahisi utambulisho wa msemaji kutambulika, yaani msemaji atakuwa ni jamii lugha ya wameru. 

ii. KIIMBO. 
Kwa mujibu wa Massamba, Kihore, na Msajila (2004), kiimbo ni umbo la sauti linalotokana na mpando-shuko wa sauti za lugha wakati wa usemaji. Katika muktadha huu wa usemaji, kila lugha ya binadamu ina utaratibu wake wa upandaji na ushukaji wa mawimbi ya sauti zake. Aidha katika utaratibu wa usemaji, dhana ya kiimbo huandamana pia na dhana ya kidatu. 

Kwaa upande wa wameru, dhana ya kiimbo huchukuwa nafasi hasa pale mtoto anapomtaja mzazi (baba au mama) au mtu yeyote anapotaja jina la mzazi kwa jina la mwanaye. Hapa kidatu hasa cha juu huchukuwa nafasi zaidi. 
Mfano; 
1. baba 
2. mama Godi 

iii. WAKAA. 
 Mgullu (2010), anasema wakaa ni ule muda ambao hutumika kutamka foni fulani. Yeye anendelea kusema kuwa, mara nyingi foni huwa na wakaa wa aina tatu: wakaa wa kawaida, wakaa mfupi kuliko kawaida na wakaa mrefu kuliko kawaida. Katika baadhi ya lugha wakaa huwa ni sifa bainifu ya lugha hiyo, kwa hivyo, watumiaji huteua wakaa unaowafaa. 
 Kwa wameru, wakaa unaotumika sana ni wakaa mrefu. Matumizi ya wakaa huu hujitokeza hasa pale baadhi ya majina ya watu yanapotajwa kwa kufupishwa. 

Mfano; Godi (godfrey) /godi:/ Johnso (johnson) /jonso:/
Matamshi ya aina hii ni ya kawaida kwa mmeru na yanamtambulisha popote pale nchini Tanzania.


 iv. MKAZO.  
Kwa mujibu wa Massamba na wenzake (2004), mkazo ni utamkaji wa nguvu zaidi katika sehemu ya neno au katika fungu la maneno. Kwa kawaida huu utamkaji wa nguvu hufanywa kwenye silabi. Silabi inayotamkwa kwa mkazo huwa na msikiko mkubwa zaidi kuliko silabi nyingine za neno hilo. 
 
Dhana ya mkazo hujitokeza kwa namna mbili yaani mkazo katika kiwango cha neno na katika kiwango cha sentensi. Aidha katika Kiswahili kwa kawaida mkazo hufanyika katika silabi ya mwisho kaso moja. Katika lugha ya kimeru mkazo hufanyika katika silabi ya mwisho na ni katika kiwango cha neno hasa katika utamkajia wa majina ya watu. 
 Mfano; 
1. Mama, 
 2. Chacha, 
 3. Baba. 
Katika namna hii ya utamkaji wa mkazo, ni rahisi kumtambua mmeru katika mazingira yoyote yale. 


v. UFUPISHAJI WA MANENO. 
Ufupishaji ni usemaji au utamkaji wa baadhi ya maneno kwa kuacha sehemu ya neno au maneno hayo. Katika jamii za kimeru ufupishaji wa maneno ni jambo la kawaida pindi mawasiliano yanapochukuwa nafasi. Ufupishaji huu hujitokeza pale maneno mawili yenye maana tofauti yanapounganishwa na kuundwa kwa neno jipya. Sehemu ya neno moja au maneno mawili yanayoungana huondolewa (hudondoshwa) na muungano wa sehemu zinazosalia huungana kuunda neno jipya. Hili hujitokeza hasa katiak matamshi.  
Mfano; 
MAMA + GODIFREI = MAGODII. 
 BABA + SAURI = BASEUU. 
Katika utamkaji wa maneno (majina) hayo hapo juu, sauti /e/ huongezwa na hivyo utamkaji wa maneno hayo huambatana na wakaa mrefu yaani /e:/. 
Mfano; 
1. Magodiee (/magodie:/) 
 2. Baseuee (/baseue:/) Hali hii hujitokeza zaidi pale mzazi anapoitwa kwa kutaja cheo chake (baba au mama) na kuunganishwa kwa kutaja jina la mtoto (Mama Godfrey, au Baba Sauri). 
Usemaji au utamkaji wa aina hii humtambulisha mmeru popote pale nchini Tanzania. 



UDONDSHAJI NA UKIUSHII. UDONDOSHAJI; 
Hapa tunarejelea dhana inayohusu uachaji wa baadhi ya vitamkwa wakati wa uandishi au usemaji wa sauti fulani. 

 UKIUSHI; 
Hapa tunarejelea hali ya kwenda kinyume na utaratibu wa kawaida (wa msingi) au uliozoeleka katika usemaji au uandishi yaani utaratibu wa kisarufi unakiukwa aidha kwa makusudi au bila kujua. Wazungumzaji wa jamii lugha ya kimeru hutumia dhana zote mbili katika utamkaji wa baadhi ya sauti. Mfano: baadhi ya sauti hudondoshwa na nyingine kupachikwa pasipostahili kuwekwa. 

1. Hapana hutamkwa apana. Hapa sauti /h/ imedondoshwa. 
2. Asubuhi hutamkwa hasubui. Hapa sauti /h/ imebadilishiwa eneo la kuka matamshi na otografia.  
3. Uumbaji hutamkwa huumbaji. Hapa sauti /h/ imepachikwa pasipoistahili. 
Kwa ujumla, maneno yanayoanza na irabu (a,e,i,o,u) hupachikwa sauti /h/ mwanzoni mwa neno hilo hata kama haistihili kuwepo (kama mfano wa 3). 
Pia silabi yoyote inayoundwa na sauti /h/+irabu yoyote (ha, he, hi, ho, hu), sauti /h/ hudondoshwa na kuachwa irabu peke yake (kama mfano wa 1 na wa 2). 
Huu ni utaratibu wa kawaida wa utamkaji kwa jamii lugha ya kimeru na hivyo ni sehemu ya utambulisho wao katika lugha. 



HITIMISHO.
Pamoja na kuwa lugha peke yake haiwezi kumtambulisha mzungumzaji, bado hakuna ubishi katika hili kuwa lugha ni kibainishi cha msingi cha utambulisho wa mzungumzaji kwani lugha ya mzungunzaji na utambulisho wake ni vitu viwili visivyoweza kutenganishwa. 
Hii ni kwa sababu matamshi ya msemaji ni utambulisho wake kwa hakika.




MAREJEO: 
Massamba, D.P.B, Kihore, Y.M & Msanjila, Y.P (2004), Fonolojia ya Kiswahili sanifu. Taasisi ya uchunguzi wa Kiswahili (TUKI). Chuo kikuu cha Dar es salaam. Mgullu, R.S (2010), Mtaala wa isinu; Fonetiki, Fonolojia, na Mofolojia ya Kiswahili. Longhorn Publishers Ltd. Nairobi, Kenya. Tabouret, K, & Andree, L. P (1986). The mother tongue metaphor. Grazer Linguistische Studien 27: 249-259.



PAKUA APPLICATION YETU(Google Playstore)


Don't forget to leave your comment on our service......................