ACHANA na kipigo walichopata Tanzania Prisons dhidi ya Yanga na kutupwa nje kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC), kocha mkuu wa timu hiyo Abdalah Mohamed ‘Baresi’ amesema watakutana tena Sokoine na kulipa kisasi.

Prisons juzi Ijumaa ikicheza kwenye Uwanja wa Azam Complex ilikumbana na kipondo cha mabao 4-1 dhidi ya bingwa huyo mtetezi kwenye kombe la FA na ligi kuu na kuondoshwa hatua ya 16 bora.
Pamoja na matokeo hayo, timu hizo zinatarajia kukutana tena kwenye mchezo wa mwisho wa kufunga msimu wa Ligi Kuu, Mei 28 mwaka huu kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini hapa.
Baresi alisema pamoja na kwamba walitamani kufika mbali lakini hesabu hazikwenda vizuri na kujikuta wakitupwa nje na sasa wanaelekeza nguvu mechi za ligi ili kukwepa kushuka daraja.
Alisema licha ya Yanga kushinda mechi hiyo lakini vijana wake walionesha soka safi licha ya kucheza pungufu na kwamba watakutana tena Sokoine na watalipa kisasi na kuwaomba mashabiki kuwa na uvumilivu.
“Tunaenda kujipanga upya na michezo ya ligi kuu tukianza na Namungo Machi 11 ugenini, kisha kurudi nyumbani dhidi ya Ruvu Shooting, lakini kama haitoshi Yanga tutakutana nao tena Sokoine mechi ya kufunga msimu lolote linawezekana,”
“Niwaombe mashabiki na wadau wa Prisons kuwa na subra benchi la ufundi linaendelea kufanya mipango kuhakikisha hatushuki daraja kwa kushinda mechi zilizobaki,” alisema Baresi.
Nahodha wa timu hiyo, Benjamin Asukile alisema mechi sita walizonazo kumaliza ligi ni za kufa na kupona na kwamba matokeo yaliyopita ni kuyasahau na kujipanga upya ambapo Prisons inashika nafasi ya 14 ikicheza mechi 24 na kukusanya pointi 22 hadi sasa.
“Sisi wachezaji tuko fiti hatujakata tamaa na hesabu zetu ni kushinda mechi zote zilizobaki na kuwa salama, yaliyopita yamepita tunaangalia yajayo,” alisema Asukile.