SHUJAA aliyeivusha Yanga kutinga makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa bao alilofunga ugenini nchini Tunisia dhidi ya Club Africain, Stephane Aziz KI ametoa kauli ya kibabe akiwaambia mashabiki wa timu hiyo kuwa watawapa raha zaidi leo kwa kuivusha timu kwenda robo fainali.

Leo kuanza saa 1:00 usiku Yanga itashuka Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam kuvaana na US Monastir pia ya Tunisia katika mechi ya Kundi D ya Kombe la Shirikisho na ushindi wa aina yoyote utaivusha kwenda robo fainali.

Kutokana na kutambua umuhimu wa mchezo huo, Aziz KI alisema mastaa wa Yanga wanashuka uwanjani leo wakiwa na akili moja ushindi wa pointi tatu kwa lengo la kuivusha timu kwenda robo, lakini kuwapa raha wanachama, mashabiki na wapenzi wa timu hiyo.

Akizungumza na Mwanaspoti, Aziz KI mwenye mabao matano katika Ligi Kuu Bara alisema wanajua umuhimu wa mchezo huo kama fainali na wamejipanga ili kutowaangusha wana Yanga.

“Tunakwenda kusaka pointi tatu haitakuwa rahisi, ila mipango ndio hiyo pia ni mchezo wa kulipa kisasi kwa Monastir waliotufunga ugenini kwenye mchezo wa kwanza. Hii ni mechi yenye heshima kubwa kama wana Yanga, lakini kwa sisi wachezaji na benchi la ufundi,” alisema Aziz Ki na kuongeza:

“Kila mchezaji anatambua umuhimu wa mchezo huo na tunatamani kuingia kwenye rekodi nyingine baada ya kuweza kufanya makubwa ugenini kwenye mchezo uliotufikisha hatua hii tuliyopo sasa. Kila kitu kinawezekana.”


DENI LA YANGA

Nyota huyo aliyesajiliwa na Yanga msimu huu kutoka ASEC Mimosas ya Ivory Coast, alisema tangu amejiunga na timu hiyo bado hajaonyesha ubora wake kutokana na kukosa ujasiri wa kucheza kwa kujiamini kulikotokana na ugeni na anajua deni kubwa alilonalo kwa mashabiki wa klabu hiyo.

“Nina deni na wana Yanga msimu huu unaoelekea mwishoni. Sijafanya kazi kwa ukubwa niliotarajiwa baada ya kuzoea ligi ya Tanzania narudi kujipanga kwa msimu mpya ili nifanye kazi kwa ukubwa zaidi,” alisema Aziz KI.

“Nafurahia maisha ya Yanga wachezaji ni wakarimu na ni wepesi wa kumuelekeza mtu pale anapoonekana hajafanya kile kinachotakiwa bila kusubiri kocha azungumze. Soka la kisasa lipo hivyo mchezaji akielewa kile anachoambiwa na mwenzake uwanjani anatengeneza ubora.”

Alisema amekuta timu ina muunganiko na yenye wachezaji imara wanaompa changamoto ya kujituma zaidi ili aweze kupata nafasi ya kucheza dakika anazopata ziendelee kumjenga na kumuingiza kwenye mfumo wa timu hiyo.

“Sio rahisi kuonyesha ubora kwenye kikosi kipya, kwani kuna utofauti mkubwa wa mifumo nilikotoka na nilipo sasa. Pia aina ya uchezaji wangu haiwezi kuwa sawa na wengine lakini nashukuru wameanza kunielewa na wamekuwa wakinielewesha nini natakiwa kufanya ili kuweza kufikia malengo ya timu na benchi la ufundi.”


JOIN OUR SOCIAL MEDIA PLATFORMS FOR DAILY UPDATES

JOIN OUR WHATSAPP GROUP  

👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇






TAP HERE TO JOIN OUR TELEGRAM CHANNEL


TAP HERE TO VISIT OUR WEBSITE


TAP HERE TO DOWNLOAD OUR APP (GOOGLE PLAY STORE)


Please leave your comment