Klabu ya Horoya ya nchini Guinea ambayo ndiyo wapinzani wa Simba kwenye mchezo wa kwanza wa Makundi Klabu Bingwa Barani Afrika wamefungiwa kuchezea katika uwanja wao wa nyumbani Stade du 28 Septembre wenye uwezo wa kubeba mashabiki 25,000.

Maamuzi hayo yametolewa na Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) baada ya kubaini kuwa Uwanja huo haujakidhi vigezo kama ambavyo shirikisho hilo lilielekeza hivyo kwa sasa Horoya watalazimika kwenda kutumia viwanja vya Senegal ama Mali.

Mratibu wa Simba, Abass Ally ambaye yupo Conakry nchini Guinea amesema; “Hali ya hewa ya Guinea haitofautiani kabisa na ile Dar es Salaam ambapo ni nyuzijoto 28-30, hata mvua zinazonyesha Dar na huku zinanyesha vilevile na huu mji tulipo, Conakry ni mji ambao upo kwenye mwambao wa Bahari kama Dar.

“Horoya wanasema kwao itakuwa mechi ngumu kwa sababu wanakwenda kukutana na miongoni mwa timu bora za Afrika kwa sasa.

“Mechi hii Horoya hawatacheza na mashabiki, kwa sababu wamefungiwa uwanja wao, lakini kwa kuwa muda ulikuwa mchache wakaruhusiwa kucheza mechi moja tu ya Simba lakini mechi zijazo watachezea Senegal au Mali.

“Horoya nao ni timu ngumu, na wanacheza Ligi ya kwao lakini tangu Januari 21 wamesimama hawajacheza mechi yoyote, walipewa mapumziko na chama chao cha Soka ili waweze kujiandaa na mechi hizi za mashindano ya CAF.

“Kwa upande wetu Simba kila kitu kipo sawa kwa asilimia 95 mpaka sasa na mchezo utachezwa kesho majira ya saa 10:00 kwa saa za Guinea lakini ni sawa na saa 1:00 jioni kwa saa za Afrika Mashariki,” amesema Ally.