Kikosi cha Simba kimepaa alfajiri ya jana kwenda Guinea kuifuata AC Horoya ya Guinea katika mechi ya ya Ligi ya Mabingwa Afrika, huku kocha mkuu wa timu hiyo, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ akiwapa kazi maalumu mabeki wake wa kati Henock Inonga na Joash Onyango.

Kocha huyo ameshtuka kuwa, kumekuwa na makosa madogo madogo yanayofanywa na mabeki hao na fasta amewakalisha kikao na kuwaeleza hataki kuona wakijichanganya tena au kuleta mzaha kwani wanaweza kuiponza timu kwenye mechi hiyo ya ugenini ya Kundi C na zitakazofuata.

Akizungumza, Robertinho alisema anaijenga Simba kuwa imara kwenye kila eneo na kwa upande wa washambuliaji na viungo tayari ameona mwanga na sasa anapambana na mabeki wa kati kina Onyango na Inonga kuhakikisha wanatengeneza ukuta imara zaidi.

“Timu iko kamili kila eneo, lakini hatujamaliza bado, sasa nimeelekeza nguvu zaidi eneo la ulinzi kutokana na baadhi ya makosa niliyoyaona kwenye mechi za hivi karibuni.

Inonga amepona na nataka acheze mchezo ujao sambamba na moja ya mabeki waliopo ndio maana nilimpa nafasi kwenye mechi mbili zilizopita ili apate utimamu wa mchezo na awe tayari dhidi ya Horoya,” alisema Robertinho na kuongeza;

“Pamoja na hayo bado kuna kitu nimekigundua, kuna nyakati mabeki wakati wanakosa mawasiliano mazuri jambo ambalo sitaki litokee tena na nimeanza kulifayia kazi, awe Onyango, Inonga, Kennedy (Juma), na Ouattara (Mohamed) au yeyote yule atakayecheza eneo hilo sihitaji kumuona akifanya makosa.”

Robertinho pia aliweka wazi licha ya kwamba watacheza ugenini, lakini anahitaji ushindi na kutoruhusu bao ndio maana amekomaa zaidi na mabeki.

“Mpango wetu ni kushinda ugenini na kutoruhusu bao, hauwezi kufanya hivyo bila kuwa na timu imara ndio maana nataka hadi kufika siku ya mechi tuwe tumeweka kila kitu sawa.

Wafungaji wanafanya vizuri na wanafunga, hivyo hivyo kwa viungo na mabeki lakini nataka kitu cha ziada kiongezeke zaidi ya wanavyofanya sasa, kwani Ligi ya Mabingwa ni ngumu zaidi,” alisema Robertinho aliyefunguka kutembea na faili la Horoya akiwatazama wanavyocheza ili aweze kupata alama tatu ugenini.

Simba itajitupa uwanjani kesho kutwa, Februari 11, na baada ya hapo itarudi nyumbani akuisubiri Raja Casablanca ya Morocco mechi inayotarajiwa kupigwa Februari 18 mwaka huu na kisha Vipers ya Uganda.